1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Biashara Duniani yako hatarini

Othman, Miraji29 Julai 2008

Muwafaka uko mbali kuhusu Biashara ya Dunia

https://p.dw.com/p/Em9Y
Makamo wa waziri mkuu wa Kenya na waziri wa biashara, Uhuru Kenyatta, akizungumza katika mkutano wa Shirika la Biashara Duniani mjini Geneva.Picha: AP

Mazungumzo ya kuyanusuru maafikiano juu ya mfumo wa biashara wa dunia yalikaribia kuvunjika leo kutokana na hatua zanazokusudia kuzisaidia nchi maskini kuwalinda wakulima wao. Nchi zinazoendelea, kama vile China na India, zinagongana na nchi muhimu zinazosafirisha vyakula, kama vile Marekani, juu ya suala la kuweka ulinzi dhidi ya mmiminiko mkubwa wa mazao ya vyakula kutoka nchi za nje. Pia kuna tafauti juu ya sehemu za kimsingi za mapatano ambazo pia hazijasuluhishwa.

Leo ni siku ya tisa ya mazungumzo hayo ya Geneva yaliopewa jina la Duru ya Doha, na mawaziri wa biashara wa nchi nyingi duniani walikuwa wanajaribu kuyasuka mapatano, japokuwa maafisa wanasema kuna uwezekano wa mazungumzo hayo kushindwa. Madhumuni ni kuiokoa duru ya mazungumzo ya Doha iliodumu sasa miaka saba, na hadi sasa hakuna ishara kwamba kutaambuliwa muwafaka mpya. Mkutano huo wa sasa wa Geneva wa nchi zanachama muhimu 30 ta Shirika la Biashara Duniani, WTO, muda wake umesharefushwa mara kadhaa kukitarajiwa kutafikiwa makubaliano, lakini waziri wa biashara wa Indonesia, Marie Elka Oangestu, amesema baadhi yao wako tayari kubakia huko Geneva kwa muda mrefu kama utakaochukuwa; wako tayari kubakia kwa siku chache zaidi, ikiwa ni lazima. Maafisa hao wanatakiwa wakubaliane juu ya masharti kadhaa ya kupunguza ruzuku zinazotolewa kwa wakulimapamoja na bei za mazao ya kilimo na yale ya viwandani.

Mashauriano hayo ya kupatikana muwafaka juuya biashara ya dunia nzima na kuondosha vizingiti yalianza mwaka 2001, muda mfupi baada ya mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11 yaliofanywa Marekani, kwa matarajio ya kuupiga jeki uchumi wa dunia na kuzisaidia nchi maskini. Mazungumzo hayo yamejikokota kwa miaka, na sasa kuna hatari ya kucheleweshwa kutokana na uchaguzi ujao wa urais huko Marekani pamoja na mambo mengine. Maafisa kutoka Marekani, China na India walibakia na ukaidi wao kuhusu suala la kuweko utaratibu maalum wa kujilinda dhidi ya mmiminiko mkubwa wa mazao ya vyakula, kama vile mchele.

China, ambayo ni msafirishaji mpya mkubwa wa mazao ya kilimo, na ambayo inashiriki katika mazungumzo haya ya Shrika la Biashara Duniani, WTO, kwa mara ya kwanza imeituhumu Marekani kwamba inatoa madai ya kupita mipaka kwa nchi zinazoendelea. Waziri wa biashara wa Uchina, Chen Deming, alisema Marekani inatoa maombi yalio ya juu kama mbingu. Nazo nchi za Umoja wa Ulaya zinataka zipatiwe masharti yalio bora kwa biashara yake. Lakini Ujerumani inapendelea kupatikane muwafaka. Ufaransa imeonya kwamba mapatano ya mwisho kutokana na pendekezo la sasa huenda yakakataliwa mwakani na nchi za Ulaya. Waziri wa uchumi wa Ufaransa, Christine Lagarde, alisema wao huko Ufaransa na Ulaya hawatakubali tu kuacha wazi milango ya nchi zao na kuwachia miaka 14 ijayo kwa Wachina kujitayarisha kana kwamba nchi yao ni inayochipuka.

Naye waziri wa sheria wa Japan ameitaka nchi yake isimame kidete katika mazungumzo hayo ya Geneva, akionya kwamba nchi hiyo ya Asia yenye uzito wa kiuchumi huenda mwishowe ikakabiliana na njaa pindi kutapatikana muwafaka mbaya huko Geneva. Kunio Hatoyama ikiwa nchi yake itaregeza kamba huko Geneva ambayo yatawaumiza wakulima wake, basi jambo hilo litapelekea wan anchi wa Japan kufa kw anjaa baada ya miaka 20 hadi 30 kutoka sasa. Lichaya Japan kuwa na hamu sana ya kuwalinda wakulima wake, nchi hiyo inaagiza kutoka nje asilimia 60 ya mahitaji yake ya vyakula. Nchi hiyo inataka mwanzoni ilitaka asilimia 10 ya mazao yake ya kilimo yalindwe katika kupunguzwa bei.