1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya biashara duniani yasambaratika mjini Potsdam

22 Juni 2007

Mazungumzo ya biashara baina Umoja wa Ulaya, Marekani,Brazil na India yamesambaratika mjini Potsdam kutokana na nchi hizo kutofautiana juu ya masuala ya ushuru na ruzuku.

https://p.dw.com/p/CB3N
Picha: DW / Anuj Chopra

Mazungumzo hayo ya nchi wanachama wa shirika la biashara duniani WTO yalikuwa na lengo la kuendeleza mchako wa mageuzi katika biashara ya dunia. Kusambaratika kwa mazungumzo hayo mjini Potsdam kunaleta mashaka zaidi katika mchakato wa juhudi za Doha.

Wawakilishi kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya, Brazil na India wameshindwa kuafikiana juu ya masuala ya ushuru na ruzuku.

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil bwana Celso Amorim alisusa na kuondoka kwenye mkutano wa mjini Potsdam mashariki mwa Ujerumani. Waziri Amorim amesema hapakuwa na faida yoyote kundelea na mazungumzo hayo kwa kuzingatia ajenda iliyokuwapo.

Waziri huyo ameeleza kuwa suala la ruzuku ndilo lililosababisha kusambarika mazungumzo hayo. Mjumbe wa India pia alisusia mkutano.

Nchi zinazoendelea zinazitaka Marekani na Umoja wa Ulaya zipunguze ruzuku zinazotolewa kwa wakulima ili nchi zinazoendelea nazo zifungue masoko yao kwa bidhaa za nchi za viwanda.

Kushindikana kwa mazungumzo ya mjini Potsdam kutafanya iwe vigumu kwa wanachama 150 wa shirika la biashara dunaini WTO kufikia mapatano hadi kufikia mwishoni mwa mwezi ujao katika mchakato wa Doha wenye lengo la kuwaondolea umasikini mamilioni ya watu katika nchi zinazoendelea.

Akizungumzia juu ya mkutano wa mjini Potsdam kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya bwana Mendelsohn amesema kuwa nchi za Ulaya haziwezi kuendelea kutoa tu bila ya nazo kupata kitu kutoka kwa nchi zinazoendelea.

Hatahivyo mkurugenzi wa shirika la biashara duniani WTO bwana Pascal Lamy ameeleza matumaini juu ya kufikiwa mapatano katika siku za usoni.