1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuunda serikali Ujerumani yatatizika

29 Januari 2018

Mazungumzo ya muungano baina ya vyama vya kihafidhina vya CDU/CSU na chama cha Social Demokratic SPD yemetatizika kutokana na mvutano juu ya masuala ya uhamiaji na afya.

https://p.dw.com/p/2rgWn
Deutschland Sondierungsgespräche in Berlin Merkel und Schulz
Picha: Reuters/H. Hanschke

Mazungumzo hayo yalianza bila ya kuonekana ukaribiano mkubwa katika masuala hayo yenye utatanishi baina ya chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU na chama ndugu cha CSU pamoja na chama cha Social Demokratic SPD.

Chama cha SPD kinataka kujadiliwa upya suala la kuwaruhusu ndugu wa wakimbizi kuja Ujerumani kuungana na jamaa zao katika kipengele wanachokipendekeza cha ‘'Shida'' ambapo wahusika wataungana na familia zao za msingi yaani wanandoa, wazazi na watoto wao wadogo au watoto wanapokuwa hapa Ujerumani basi wazazi wao waruhusiwe kuungana nao. Chama cha SPD kinataka kanuni hiyo ijadiliwe upya kabla ya kufikia makubalino ya kuunda serikali ya mseto lakini pendekezo hilo linapingwa na vyama vya CDU na CSU.

Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz
Kiongozi wa chama cha SPD Martin SchulzPicha: Reuters/C. Mang

Kiongozi wa chama cha SPD Martin Schulz amesema chama chake kinataka kuingia kwenye serikali ya muungano iliyoundwa kwa  msingi madhubuti. Bunge la Ujerumani  litaamua  alhamisi ijayo juu ya suala la wakimbizi  wanaoweza kuwaleta jamaa  zao nchini Ujerumani. Bwana Schulz amesema hata hivyo vyama hivyo vimeweza kupiga hatua katika suala la kilimo.

Mjumbe wa chama cha CSU Joachim Hermann amemtaka kiongozi wa  chama  cha SPD  Martin  Schulz azingatie zaidi maslahi ya nchi badala yale ya chama chake. Bwana Hermann ambaye ni  waziri  wa mambo ya ndani  wa  jimbo la Bavaria la kusini mwa Ujerumani ameliambia gazeti la Passauer Neuen Presse la hapa Ujerumani kwamba haiwezekani iwe ni upande wa vyama vya CDU na CSU tu unaokubali mengi  zaidi. Chama cha CSU kinataka idadi ya wakimbizi wanaoruhusiwa nchini Ujerumani isivuke 220,000 kwa mwaka.

Mnadhimu mkuu wa chama cha CDU Peter Altmaier
Mnadhimu mkuu wa chama cha CDU Peter AltmaierPicha: picture alliance/dpa/W. Kumm

Mnadhimu mkuu wa ofisi ya kansela bwana Peter Altmaeir wa chama cha CDU amesema leo alfajiri baada ya vikao vya wajumbe 15 wa vyama hivyo vitatu kwamba mazungumzo yalikuwa ya makini sana. Bwana Altmaeier amesema licha ya tofauti zilizopo katika masuala ya msingi pande zote zimesisitiza kwamba zipo tayari kufikia mwafaka.

Pande zote za CDU/CSU na SPD zimekubaliana kuipa jukumu kamati maalum kulishughulikia suala hilo katika siku nzima ya leo ili kutafuta kigezo cha suluhisho.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/ p.dw.com/p/2rgEI

Mhariri: Gakuba, Daniel