Mazungumzo ya Shirika ya biashara duniani WTO.
27 Mei 2004Wajumbe kutoka nchi zinazoendelea katika mazungumzo ya Shirika la biashara duniani-WTO-wanasema kwamba hatima ya yaliopendekezwa katika kile kinachojulikana kama awamu ya Doha bado imo hatarini,kwa kuwa matokeo yake yanachukua muda mrefu kuzaa matunda. Katika majadiliano ya shirika hilo miaka mitatu iliopita kuhusu suala la kuwapatia madawa wakaazi wa nchi masikini kwa bei ya chini na hasa zile zilizoko barani Afrika, kulizuka majadiliano makali. Yaliofikiwa katika mazungumzo ya Doha nchini Qatar Novemba 2001 katika mkutano wa mawaziri wa nchi wanachama yalilengwa kukamilishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, na kuanza mazungumzo kuhusu ajenda iliokubaliwa.
Mvutano ulipamba moto baada ya kuwemo pia baadhi ya masuala juu ya uhuru wa biashara kuhusika na mazao ya kilimo katika ajenda ya shirika hilo, au masuala yanayohusiana na zingatio la wapi, mji na eneo gani yanatoka mazao hayo.
Pamoja na hayo lakini hivi sasa inaelekea hali ya mambo ndani ya taasisi hiyo ya biashara ya kimataifa ni nyengine. Wajumbe kutoka takriban nchi zote 147 wanachama wamechukua msimamo imara kuelekea mazungumzo ya biashara, huku zingatio lao likituwama zaidi katika ule muda wa mwisho uliowekwa kwa utekelezaji wa yalioamuliwa na awamu ya Doha.
Kwa mujibu wa makubaliano ya mkutano wa mawaziri wa Novemba 2001 katika mji mkuu wa Qatar yaliopelekewa kupewa jina hilo la Awamu ya Doha, mazungumzo yangepaswa kukamilishwa ifikapo mwisho wa mwaka huu- lakini hadi mwishoni mwa mwezi Julai mataifa wanachama yatapaswa kukamilisha muundo wenyewe wa majadiliano na hasa kuhusiana na biashara ya mazao ya kilimo, suala lililokua mwiba wa mchongoma miongoni mwa masuala yaliomo katika ajenda ya mazungumzo ya Doha.
Wadadisi na hasa wa jumuiya za kiraia zinazofuatilia mazungumzo hayo, wanasema kinachohitajika ni juhudi zaidi za kuleta maridhiano kati ya wajumbe.Baadhi wanaashiria kwamba ikiwa Marekani na Umoja wa ulaya hazionyeshi nia yoyote ya kisiasa, ajenda ya Doha itashindwa.
Marekani na Umoja wa ulaya pamoja na Japan na nchi chache nyengine zilizoendelea kiviwanda zinaunda kundi ambalo linaelekea kuyawekea pingamizi madai ya biashara ya mazao ya kilimo..
Afisa mkuu wa umoja wa ulaya katika mazungumzo ya WTO Carlos Torjan amesema mikutano ya mwezi Juni kuhusu biashara ya mazao ya kilimo- wiki ya kwanza na ya mwisho ya mwezi huo itakua na umuhimu mkubwa.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Supachai Panitchpakdi –akizungumzia juu ya hali ya mazungumzo, amesema mazingira ya kisiasa yamebadilika sana hivi sasa na kwamba mazungumzo ya biashara yatashawishiwa bila shaka yoyote na matokeo ya mikutano ijayo ya mawaziri kama vile wa umoja wa Afrika mjini Kigali na wa Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Asia na eneo la bahari ya Pacif-APEC. Lakini mkurugenzi huyo mkuu wa WTO akaonya juu ya kuwa na matumaini makubwa mno, akiongeza kwamba bado kuna matatizo magumu kadha wa kadhaa.
Rais wa Shirikisho la kimataifa la watoaji mazao ya kilimo, Jack Wilkinson anakubaliana na maoni hayo ya Bw Supachai akiongeza kwamba itakua vigumu kupata maafikiano juu ya mkataba wa biashara ya mazao ya kilimo, kabla ya uchaguzi wa Rais nchini Marekani mwezi Novemba.
Mbali na vikwazo vinavyoyakabili mazungumzo ya kimataifa yanayoongozwa na shirika la biashara duniani, kamishna wa biashara wa umoja wa ulaya Pascal lamy anakiri pia kwamba hata mkataba wa kibiashara unaojadiliwa kati ya kundi la ulaya na soko la pamoja la mataifa ya Amerika kusini-Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay, hauwezi kukamilishwa hivi karibuni.
Brazil ambayo pia ni mratibu wa kundi linalojulikana kama G20 la nchi zinazoendelea, likiongozwa na China, India na Afrika kusini, inatoa mchango muhimu katika mazungumzo ya biashara ya Shirika la biashara duniani na pia katika mazungumzo ya biashara ya kanda ya Amerika kusini baina ya nchi za kanda hiyo na umoja wa ulaya.
Bw Lamy alisema umoja wa ulaya unasubiri jibu hivi sasa kutoka nchi hizo la G20, ambamo 17 miongoni mwao ni nchi zinazosafirisha nje mazao ya kilimo na ambazo zinapinga mtindo wa umoja wa ulaya kufidia wakulima wao pamoja na aina nyengine za kujilinda kibiashara.
Miongoni mwa yanayodaiwa na nchi zinazoendelea ni pamoja na kuondoshwa kwa viwango vikubwa vya ushuru. Kwa mfano mtindo unaotumiwa na Japan wa kuweka viwango vya juu vya ushuru kwa mchele unaotoka nchi za nje, ikiwa ni katika mbinu ya kuwalinda wakulima wake wa zao la mbunga.