Mazungumzo ya Sudan Kusini hatihati
12 Februari 2014Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko katikati mwa mwezi Desemba mwaka uliopita, wakati mapigano yalipoibuka kati ya wanajeshi watiifu kwa serikali na waasi wanaomuunga mkono makamu wa zamani wa rais. Maelfu wameuawa katika ghasia zilizofuatia, ambazo zilichukua mwelekeo wa kikabila.
Mwezi uliopita pande hizo zilikubaliana kusitisha mapigano mjini Addis Ababa, na mazungumzo zaidi yalikuwa yamepangwa kuanza tena siku ya Jumatatu, lakini hilo halikutokea. Hafla ilifanyika jana Jumanne, kwa matumaini ya kuanza mazungumzo hayo, lakini badala ya kuanza mazungumzo, pande mbili ziliutumia mkutano huo kushutumiana.
Kila upande unaulaumu mwingine
Mjumbe wa majadiliano kutoka serikali ya Sudan Kusini alisema waasi wanakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano. Kwa upande wa waasi, Jenerali Taban Deng Gai alielezea kusikitishwa kwake na rais Salva Kiir, na rais Yoweri Museveni wa Uganda. Uganda ni mshirika muhimu wa serikali ya Kiir, na imetuma mamia ya wanajeshi nchini Sudan Kusini.
Jenerali Gai alisema kuwa wanajeshi wa kigeni hawajaondolewa kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa kusitisha mapigano, na kuongeza kuwa Uganda inafanya kama vile mkoloni mpya wa Sudan Kusini. Alimshtumu rais Museveni kwa kutaka kurefusha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, na kusema huo ni ubinafsi.
Msemaji wa waasi alisema mapema jana kuwa waasi wasingerudi katika mazungumzo, hadi wafungwa wa ngazi ya juu wa kisiasa waruhusiwe kuhudhuria, na vikosi vya Uganda viondoke nchini Sudan Kusini. Msemaji huyo, Yohanis Pouk, alisema wafungwa saba wa kisiasa walioko nchini Kenya hivi sasa, na wanne walioko Sudan Kusini, hawajaruhusiwa kushiriki katika mazungumzo hayo yanayofanyika nchini Ethiopia.
"Hatuondoki huko"
Uganda imetuma zana za kijeshi na wanajeshi kupigana kwa upande wa serikali ya Sudan Kusini, katika majimbo yasiyopungua matatu, yakiwemo mawili yanayochimba mafuta. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uganda, Okello Oryem, alisema nchi hiyo itaondoa tu vikosi vyake ikiwa hayo ndiyo matakwa ya serikali ya Sudan Kusini.
Museveni alitetea hatua ya kupeleka wanajeshi nchini Sudan Kusini, akisema ilikuwa muhimu kuzuwia ghasia kusambaa katika taifa hilo changa zaidi duniani. Marekani imeitolea wito Uganda kuondoa wanajeshi wake. Waziri wa mambo ya kigeni John Kerry alisema siku ya Jumanne kuwa Marekani inafanya juhudi za kidiplomasia kuzuwia machafuko na mauaji ya halaiki vinavyoweza kutokea iwapo hali itashindwa kudhibitiwa.
Suala lingine lililoongeza ugumu katika mazungumzo hayo ni madai ya wafungwa wa kisiasa kutaka kujiunga na mazungumzo hayo, si kwa upande wa makamu wa zamani wa rais, Riek Machar, lakini kama kundi la tatu, alisema mpatanishi wa mazungumzo hayo Seyoum Mesfin kutoka jumuiya ya IGAD, na kuwalaumu viongozi wa Sudan Kusini kwa kushindwa kuzuwia mgogoro huo.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape
Mhariri: Josephat Charo