Mazungumzo ya upatanishi Mashiriki ya Kati kuanza tena
10 Machi 2012Umoja wa Mataifa umesema jana Ijumaa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton na Waziri wa Mambo ya nchi za Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov watakutana katika makao mkuu wa Umoja wa Mataifa kabla ya kikao maalum cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu wimbi la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu. Washirika wengine wa majadiliano hayo - Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton na mjumbe maalum wa kundi hilo Tony Blair watachangia kupitia njia ya video.
Wajumbe wa Umoja wa Mataifa wamesema Urusi imeanza kushinikiza kuandaliwa kwa mkutano huo wa pande nne. Haikubainika ikiwa kundi hilo lilipanga kutoa taarifa ili kuhimiza kurejelewa mazungumzo hayo baina ya Waisrael na Wapalestina, suala ambalo limezungukwa na mjadala baina ya Israel na Marekani kuhusu uwezekano wa shambulizi la kijeshi dhidi ya Iran kutokana na mpango wake wa nyuklia.
Ulimwengu hauskii kilio cha Palestina
Huku wakikumbwa na mizozano ya kindani, Wapalestina wamejizatiti kupaza sauti zao zisikike katika miezi ya hivi karibuni. Macho ya ulimwengu yameangazia uchaguzi wa rais nchini Marekani, machafuko yanayoshuhudiwa nchini Syria na mpango wa nyuklia wa Iran.
Ban Ki Moon alisema mjini Jerusalem mwezi jana kuwa Israel na Wapelestina wanaishiwa muda wa kutatua mzozo wao na wanapaswa kulipa kipau mbele suala la kurejelea mazungumzo.
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, analo sharti la mazungumzo hayo, anataka Israel ikubali kuundwa wka taifa la Palestina kwenye ardhi yake yote iliyochukuliwa katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka ya 1967.
Rais wa Israel Benjamin Netanyahu amekataa kukubali ombi hilo na amepuuza masharti ya Wapalestina ya kusitisha shughuli za ujenzi wa makaazi katika ardhi ambayo Wapalestina wanataka kuwa taifa lao.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Sekione kitojo