1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya WTO yamevunjika

P.Martin30 Julai 2008

Majadiliano ya Shirika la Biashara Duniani- WTO yamevunjika baada ya Marekani,China na India kushindwa kuafikiana katika suala la ushuru wa forodha wa mazao ya kilimo.

https://p.dw.com/p/EmSn
European Union Commissioner for Trade Peter Mandelson speaks during a media conference at EU headquarters in Brussels, Thursday July 17, 2008. Troubled global trade talks are a crucial test for how a new world order can handle future world challenges such as climate change and food supply, the EU's trade chief said Thursday. Mandelson said talks between World Trade Organization nations in Geneva next week were happening at a time of "huge reordering of the global economy and politics" and would test their ability to strike a deal. (AP Photo/Virginia Mayo)
Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya,Peter Mandelson.Picha: AP

Mawaziri wa biashara waliowakilisha nchi wanachama 30 muhimu katika WTO walikutana Geneva Uswisi katika jitahada ya kukamilisha makubaliano mapya kuambatana na mazungumzo ya biashara yaliyozinduliwa Doha nchini Qatar miaka saba iliyopita.Lengo ni kuwa na uhuru zaidi katika masoko ya kimataifa na hivyo kurahisisha biashara kati ya nchi mbalimbali.

Lakini nchi zinazoendelea zinataka kuhakikisha kuwa uhuru zaidi wa kibiashara duniani hautowaathiri wakulima wao.Hilo ni suala lililosababisha mvutano na kukwamisha majadiliano huku nchi masikini na tajiri zikitupiana lawama.India na China zimepinga kufungua zaidi masoko yake ya kilimo zikihofia kuhatarisha mfumo unaowalinda wakulima wake.Zimesema kuwa zinazungumza kwa niaba ya kama nchi 100 zinazoendelea.Hata baadhi ya nchi masikini na zinazoendelea zimeunga mkono msimamo wa India na China.

Lakini mjumbe wa Marekani katika majadiliano ya WTO,Susan Schwab alizituhumu China na India kuwa zimezuia maendeleo kupatikana.Ingawa China baadae iliregeza msimamo wake.India nchi mojawapo inayoinukia kiuchumi duniani, ilisimama kidete mbele ya dola lenye nguvu kubwa za kiuchumi-Marekani.

Baadhi ya wajumbe wa WTO wameelewa msimamo wa nchi hizo mbili zinazoendelea zikiwa na jukumu la kuwafikiria wananchi wake wengi walio masikini na wamesema, usalama wa kilimo na chakula nchini India na China,unapaswa kuimarishwa na sio kudhoofishwa kwa bidhaa rahisi kutoka nje.

Kwa upande mwingine,Waziri wa Biashara wa China Chen Deming,katika tovuti ya wizara yake amesema,China sawa na nchi nyingi zingine,imesikitishwa sana kwa kutofanikiwa kwa majadiliano hayo mjini Geneva.Akaongeza kuwa ni matumaini yake kwamba wanachama wote wa WTO watatafakari na kupata somo ili majadiliano ya siku zijazo yaweze kufanikiwa.

Wakati huo huo,mpatanishi mkuu Peter Mandelson alie Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya amesema,kutofanikiwa kupata makubaliano ya mkataba mpya wa biashara duniani ni jambo la huzuni mkubwa.Hata Kamishna wa Kilimo wa Umoja wa Ulaya Mariann Fischer-Boel amesema,ni siku ya msiba mkubwa kwa nchi zinazoendelea ambazo zingeweza kunufaika kwa njia nyingi kama majadiliano hayo yangefanikiwa.

Lakini kutofanikiwa kwa majadiliano hayo hasa ni pigo kubwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa WTO Pascal Lamy.Kwani yeye alitumaini kuwa makubaliano yatapatikana kati ya nchi wanachama 135 kufuatia mivutano ya miaka saba iliyopita.