Mbio za kurundika silaha zaanza upaya
5 Februari 2018Tunaanzia na kitisho cha kuzuka upya mbio za kurundika silaha ulimwenguni. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: Baada ya mzozo kati ya kambi za mashariki na magharibi kumalizika, yalichomoza matumaini ya angalao kuwa na ulimwengu bila ya silaha za atomiki. Lakini matumaini hayo hayajakawia kufifia na badala yake idadi ya nchi zinazotangaza kumiliki silaha za nuklea inazidi kuongezeka. Nadharia mpya ya silaha za nuklea nchini Marekani inazungumzia hivi sasa kubuniwa "silaha ndogo ndogo za atomiki". Lakini na silaha hizo pia zina uwezo wa maangamizi sawa na ule wa mabomu ya atomiki yaliyopiga na kuiteketeza miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan mwaka 1945."
Haki ya walimwengu kuingiwa na hofu
Gazeti la "Der neue Tag" linachambua dhamiri halisi za mpango wa Marekani wa kutengeneza silaha mpya za nuklea na kuandika: "Mkakati wa Marekani ni dhahiri: Marekani itakapojipatia silaha hizo mpya za atomiki, mahasimu wao watabidi wazidi kuhofia kwamba zitatumika pia. Tayari katika kampeni zake za uchaguzi mwaka 2016 Donald Trump alitafuta ushauri kutaka kujua kwanini watu wanamiliki silaha za atomiki lakini hawazitumii. Pengine kuingiwa na kichaa sio jibu halisi, hata hivyo watu wana kila sababu ya kuingiwa na wasi wasi-tena mkubwa."
Mazungumzo ya kuundwa serikali Ujerumanai yamerefushwa
Muda uliowekwa hapo awali wa kukamilishwa mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano wa vyama vikuu-GroKo, kati ya vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU na wana Social Democrat wa SPD umemalizika jana, bila ya lengo lililokuwa limewekwa kufikiwa. Gazeti la "Donaukurier" linatupia jicho mazungumzo hayo na kuandika: "Wana Social democrat wanaweza kujinata na kusema wamefanikiwa kulazimisha miongoni mwa mengineyo mikataba ya kazi iboreshwe, hata kama madai yao makubwa ya kutaka mfumo wa aina mpya wa bima ya afya kwa wananchi hayakupita. Lakini mafanikio hayo yanasalia karatasini tu kwa wakati wote ule ambao bado haijulikani miradi hiyo itagharamiwa vipi. Na pindi fedha zikikosekena basi Martin Schulz na kiongozi wa kundi la wabunge wa SPD, Andrea Nahles watalazimika kutegemea hisani ya CDU na CSU.."
Miaka 14 tangu Umoja wa ulaya upanuliwe kuelekea Mashariki
Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika miaka 14 tangu Umoja wa Ulaya ulipopanuliwa kuelekea mashariki. Gazeti la Westfalenpost linaandika: "Umoja wa ulaya mpaka sasa haujafanikiwa kuushughulikia kikamilifu mpango wake mkubwa kabisa wa kujipanua uliotekelezwa mwaka 2004, pale mataifa 10 yalipokubaliwa uanachama. Na miaka mitatu baada ya Bulgaria na Rumania zilipojiunga na Umoja huo, hakuna kilichokuwa kimebadilika. Masilahi ya usalama ndio iliyokuwa sababu ya kukubaliwa uanachama mataifa ya magharibi mwa Balkan. Ni jambo linaloingia akilini. Pengine hali isingeweza kukadirika barani Ulaya kama Umoja wa ulaya ungekuwa haujapanuliwa kuelekea mashariki miaka 14 iliyopita. Hata hivyo halitakua kosa kujiuliza kama Umoja wa Ulaya unaweza kweli kudhamini utulivu katika eneo la Balkan ikiwa umoja wenyewe si madhubuti."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: gakuba, Daniel