Mbio za sakafuni kutaka kumvua madaraka rais wa Marekani
3 Februari 2020Tunaanzia Marekani ambako juhudi za kumpokonya rais Trump madaraka yake zinakurubia kumalizika katika wakati ambapo Republican na Democrats wanakutana Iowa , awamu ya kwanza ya kuwazinduwa wafuasi wao kuelekea uchaguzi mkuu unaokuja. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika:"Karata zimeshachanganywa. Kitakachofuatia katika mchakato wa kumpokonya rais madaraka yake wiki hii hakitakuwa na uzito wowote. Kura ya baraza la Seneti kupinga mashahidi ziada kusikilizwa inamhakikishia rais Trump hana hatia.
Wakitiwa kishindo na ofisi ya rais, warepublican wameshikamana. Wamejenga ukuta unaowatenga na hoja za kimsingi. Jamii wanataka nini, si muhimu kwao. Robo tatu ya Wamarekani wanahisi ingekuwa vizuri mashahidi zaidi kusikilizwa. Mchakato huu unabainisha, chama ambacho wakati mmoja kilikuwa kikijifakharisha kama "Grand Old Party" au chama kikubwa cha zamani", kimaadili kimeishiwa. Wawili tu majasiri ndio waliojitokeza. Hiyo ni dalili mbaya kwa mfumo madhubuti wa kidemokrasi.
Virusi vya Corona vyatishia uchumi
Idadi ya wahanga wa homa inayosababishwa na virusi vya Corona inazidi kuongezeka.Wahanga wameripotiwa pia nje ya mipaka ya China. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linazungumzia juhudi za serikali ya China kuepusha janga hilo lisiathiri pia sekta ya kiuchumi. Gazeti linaendelea kuandika: Asubuhi ya Ijumatatu, benki kuu ya China imemimina kwa mara nyengine tena Euro bilioni 156 katika mfumo wa fedha ili kuwatuliza wahusika wote-licha ya picha za kuchusha za watu waliofunga barakoa mdomoni.
Lakini kitatokea nini pindi wawekezaji wengi wakipoteza subira kwa wakati mmoja? Na kama watu watafikiri dawa ya kuzuwia maradhi yasienee inaweza pia kupatikana pindi utaratibu jumla wa uzalishaji na ugavi ukibidi kusitishwa? Mzozo wa virusi unawezaa kuleta madhara makubwa zaidi kuliko yale ya kitabibu. Unaweza hatua baada ya hatua kuuvuruga mfumo jumla wa kiuchumi ulimwenguni.
Waziri mkuu wa Uingereza atakiwa atekekeze ahadi za Brexit
Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha njia panda iliyokuwa ikiiunganisha Uingereza na Umoja wa Ulaya. Gazeti la "Frankenpost" linamulika kile kitakachofuata baada ya Brexit. Gazeti linaendelea kuandika:
"Katika wakati ambapo Boris Johnson anawahadaa wafuasi wake,bila ya Umoja wa Ulaya hali itakuwa bora zaidi, katika jimbo la Scottland sauti zimehanikiza watu wanadai uhuru. Na Ireland ya kaskazini pia wakatoliki wanatetea kuungana upya jimbo hilo na jamhuri ya Ireland. Johnson ameitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya lakini kishindo kikubwa zaidi kinamsubiri atakaposhindwa kutekeleza ahadi alizotoa. Ingawa hajali kwasababu mchezo ameshauzoweya.