Mbio za ubingwa kati ya BVB na Bayern ni kali
28 Januari 2019Mbio za kuelekea katika ubingwa zimeanza kushika kasi mapema msimu huu , wakati timu mbili zilizoko juu ya msimamo wa ligi, zikionesha nia yake ya kunyakua ubingwa huo. Mabingwa mara sita mfululizo katika Bundesliga Bayern Munich baada ya kuonekana kuwa haina mshindani katika ligi hii, mara hii imeachwa nyuma na Borussia Dortmund katika mchezo wa 19 wa Bundesliga, wakati BVB ikiwa mbele kwa pointi sita.
Bayern Munich ilihakikisha mwanya huo hauongezeki kuwa pointi tisa, pale ilipofanikiwa kuikandika VFB Stuttgart kwa mabao 4-1 jana Jumapili, hali ambayo inafanya mbio hizo kuwa za kusisimua zaidi.
Wakati BVB inasema haina presha kushinda taji hilo msimu huu, Bayern ina nia ya kuonesha kwamba wao ni miamba wasioshindika na wanataka kulinyakua taji hilo. Borussia Dortmund ilichambua kama karanga Hannover 96 kwa kuishindilia mabao 5-1 siku ya Jumamosi, hali inayoonekana kuwa kikosi hicho cha kocha Lucien Favre kina nia pia kulinyakua taji hilo.
Thomas Doll kocha mpya
Mambo hayakuishia hapo baada ya kipigo hicho Hannover 96 iliyoko katika hatari ya kushuka daraja iliamua kuachana na kocha wake Andre Breitenreiter , na kumteua Thomas Doll kuwa mrithi wake katika juhudi za kuiokoa timu hiyo kushuka daraja msimu huu. Kipigo dhidi ya Dortmund siku ya Jumamosi kilikuwa cha tatu mfululizo, ikibakia katika pointi 11 na katika nafasi ya 17 sawa na timu iliyoko mkiani ya Nuremberg.
Doll ametia saini kuifunza timu hiyo hadi mwaka 2020, mkataba ambao utadumu hata katika daraja la pili iwapo timu hiyo itashuka darja. Doll mwenye umri wa miaka 52 mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, ambaye aliwahi kuzifunza Hamburg SV na Borussia Dortmund katika Bundesliga, katika miaka ya hivi karibuni aliwahi kufunza timu nchini Saudi Arabia, Uturuki na Hungary.
Bayern Munich imejiimarisha katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 42 , sita nyuma ya Borussia Dortmund. Wakati nafasi ya tatu inashikiliwa na Borussia Moenchengladbach ikiwa na pointi 39, ikifuatiwa na RB Leipzig katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 34, baada ya jana Jumapili kuirarua Fortuna Dusseldorf kwa mabao 4-0.
Bayern wamhitaji mchezaji wa Chelsea
Callum Hudson-Odoi wa Chelsea hajaweka wazi hatima yake baada ya ripoti zilizozagaa katika vyombo vya habari kwamba kijana huyo mshambuliaji wa pembeni kuwasilisha barua yake ya ombi la kutaka kuihama klabu hiyo kwa viongozi wake. Kijana huyo machachari mwenye umri wa miaka 18 alifunga bao la pili wakati mabingwa wa kombe la FA nchini England Chelsea kuishinda Sheffield Wednesday kwa mabao 3-0 katika duru ya nne ya kombe hilo katika uwanja wa Stamford Bridge jana Jumapili.
Hudson-Odoi hapo kabla alihusishwa na kuhamia katika klabu ya Bayern Munich, ambao walisema wazi jinsi wanavyomuhitaji kijana huyo anayeichezea timu ya vijana ya England.
Alipoulizwa baada ya mchezo huo kwamba huenda alicheza mchezo wake wa mwisho na Chelsea , Hudson-Odoi aliiambia BBC , "Sifahamu, siwezi kusema. Naendelea kufanyakazi kwa nguvu na huwezi kujua kile kitakachotokea."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe, rtre, dpa , ape
Mhariri: Grace Patricia Kabogo