Mchakato wa Brexit kuhodhi Mkutano wa kilele mjini Brussels
21 Machi 2019
Waziri mkuu May atakutana na viongozi 27 wa Umoja wa ulaya mjini Brussels, siku moja baada ya kutuma risala kuomba mchakato wa Brexit urefushwe hadi juni 30 inayokuja. Umoja wa Ulaya una wasi wasi kuhusu madhara ya kisiasa, kiuchumji na kijamii yanayoweza kusababishwa na mchakato wa Brexit. Mwenyekiti wa baraza la Ulaya, Donald Tusk anaesimamia mkutano huo wa kilele anasema kuna uwezekano wa kuakhirishwa mchakato wa Brexi kwa muda mfupi, lakini kwa sharti kwamba bunge la Uingereza linaidhinisha makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Umoja wa ulaya kabla ya tarehe ya kuondoka ambayo ni Marchi 29 inayokuja.
Itakumbukwa makubaliano hayo yamepingwa mara mbili na bunge la Uingereza. Waziri mkuu Theresa May anasema "wabunge sasa wanakabiliwa na chaguo la mwisho" kati ya makubaliano yake, kujitoa bila ya makubaliano, hali ambayo itaathiri uchumi wa nchi hiyo na kubatilisha mchakato wa Brexit.
Kishindo cha Brexit cha wakumba viongozi wa Umoja wa Ulaya
Kishindo kinawakaba pia viongozi 27 walisalia wa Umoja wa Ulaya ambao kwa pamoja watabidi waridhie mpango wa kucheleweshwa mchakato wa Brexit. Wengi wameshaonya waziri mkuu May anabidi atoe sababu muhimu ili maombi yake yaweze kukubaliwa.. Wakati huo huo kiongozi wa upinzani wa Labour nchinin Uingereza, Jeremy Corbyn anapanga pia kuwenda Brussels kuzungumzia mpango mbadala wa Brexit pamoja na viongozi wa Umoja wa Ulaya. Hata hivyo hakuna maridhiano yoyote yanayotarajiwa katika mkutano huo wa siku mbili wa kilele mjini Brussels.
China, Marekani na Mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa mada mkutanoni
Mada nyengine inayotarajiwa kugubika mkutano huo wa siku mbili wa kilele inahusu China. Viongozi wa Umoja wa ulaya wataandaa ratiba kwaajili ya mkutano wa kilele pamoja na China utakaoitishwa April tisa inayokuja katika wakati ambapo viongozi hao wanataka kutathmini upya uhusiano wao na nchi hiyo inayozidi kupata nguvu kisiasa na kiuchumi.
Uhusiano pamoja na Marekani sawa na mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa mada zitakazojadiliwa pia katika mkutano huo wa kilele wa siku mbili.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters/dpa
Mhariri: Sekione Kitojo