1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchakato wa kutafuta dawa ya corona umefikia wapi?

1 Juni 2021

Mwanzoni mwa mwaka 2020, wakati virusi vipya vya corona vilipoanza kuenea kote ulimwenguni, kampuni ya dawa ya Pfizer iliiunda kundi lake linalojulikana kama SWAT la wanasayansi kutafuta dawa ya ugonjwa wa COVID-19.

https://p.dw.com/p/3uIJR
Symbolbild I Coronavirus I Intensivstation
Picha: Robert Michael/dpa-Zentralbild/picture alliance

Zaidi ya mwaka mmoja baadaye, kampuni hiyo bado haijaanza kufanyia majaribio makubwa ya dawa za kumeza kwa binadamu, jambo ambalo inasema inatarajia kuanza kufikia mwezi Julai. 

Kampuni hiyo kubwa ya dawa nchini Marekani iliyoanza kwa kutafuta chanjo, pia ilitaka kutengeneza dawa ambayo itazuia kuendelea kuenea kwa maambukizo sawa na jinsi dawa ya Tamiflu inavyotumiwa kukabiliana na homa ya mafua.

Kundi hilo liliingia maktaba ya molekuli kutafuta nyenzo zisizotumika kusaidia kuanzisha kwa haraka mchakato huo. Kampuni hiyo pamoja na nyingine shindani zinazojumuisha Merck and Co yenye makao yake nchini Marekani na kampuni ya dawa ya Roche Holding AG yenye makao yake nchini Uswisi, ziko katika harakati ya kutengeneza dawa ya kwanza ya tembe dhidi ya virusi hivyo ambazo watu wanaweza kunywa kwa haraka wanapokuwa na dalili za mwanzo za ugonjwa huo.

Lengo lao la pamoja ni kujaza pengo muhimu la matibabu kwa kuwasaidia watu ambao wamepata maambukizo ya virusi hivyo hivi karibuni kuwaepusha kuwa mahututi na kuhitaji kulazwa hospitalini.

Italien Herstellung Antikörper-Cocktail gegen Covid-19
Chanjo zikiwa maabara huko ItaliaPicha: Riccardo Antimiani/ANSA/picture alliance

Lakini baada ya takriban miezi 18 tangu kuzuka kwa janga hilo la virusi vya corona, bado hakuna matibabu yanayoweza kutolewa kwa urahisi ambayo yamethibitishwa kuwa na uwezo kamilifu wa kukabiliana na virusi vya corona.

Ufanisi wa chanjo

Hii ni licha ya kutolewa kwa chanjo kadhaa dhidi ya virusi hivyo inayojumuisha moja kutoka kwa kampuni ya Pfizer na mshirika wake wa Ujerumani BioNTech SE; ambayo mnamo mwezi Desemba ilikuwa ya kwanza kupaza idhini ya matumizi nchini Marekani.

Hali ya kampuni hiyo ya Pfizer, inatilia mkazo changamoto zinazowakabili watengenezaji dawa katika kutafuta matibabu kupitia dawa za kumeza kukabiliana na virusi hivyo.

Impfen von Kindern Corona-Impfung
Utoaji chanjo unaendelea katika mataifa mengiPicha: MiS/imago images

Tofauti na chanjo ambayo inahitaji tu kusisimua mfumo wa kinga ya mwili, dawa ya vidonge inayoweza kukabiliana na virusi hivyo inapaswa kuzuia  virusi kuenea kote mwilini huku pia ikiwa na uwezo wa kutoingilia seli zenye afya.

Maafisa wakuu wa kampuni za kutengeneza dawa wanasema kuwa kupima dawa dhidi ya virusi pia ni vigumu. Dawa inapaswa kutolewa mapema wakati wa maambukizo hii ikimaanisha kutafuta watakaoshiriki katika majaribio ambao hivi karibuni walipata maambukizo ya virusi vya corona.

Watu wengi walioambukizwa virusi hivyo hupata dalili ndogo lakini utafiti unahitajika kuthibitisha kuwa dawa ina matokeo mazuri katika afya ya mgonjwa.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Pfizer Albert Bourla, amesema kuwa kampuni hiyo huenda ikatafuta idhini ya dharura nchini Marekani kwa dawa ya tembe dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 baadaye mwaka huu.

Kampuni hiyo ya Pfizer na kampuni nyingine shindani zinasema kuwa mchakato wa kutengeneza dawa hiyo umekuwa wa kasi kuliko miaka kadhaa ambayo huchukuwa kwa kawaida kutengeneza dawa ambayo inaweza kumezwa kama tembe.

Huku viwango vya maambukizi ya virusi vya corona vikiwa vimepungua katika baadhi ya mataifa, mengine yanaendelea kukabiliana na kuenea kwa haraka kwa virusi hivyo.

Na huku chanjo dhidi ya virusi vya corona ikikabiliwa na uhaba katika mataifa mengi, watu wengi duniani hawatapata chanjo hiyo kwa miaka kadhaa. Watu wengi pia wanachelea kudungwa chanjo hiyo.

Wanasayansi wanakadiria kuwa ugonjwa wa COVID-19 ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 3.5 kote duniani huenda ukawa ugonjwa wa msimu kama vile homa ya mafua.

Kwa sasa, matibabu ya pekee yanayoonesha kusaidia wagonjwa wa COVID-19 kuepuka kulazwa hospitalini ni dawa za kinga ya mwili zinazohitaji kuingizwa katika mishipa kwa muda mrefu ambazo hazifanyi kazi vizuri dhidi ya aina tofauti ya virusi hivyo vya corona.