Peter Biar Ajak asema yumo hatarini
24 Julai 2020Ajak aliwasili nchini Marekani jana jioni akiwa na mkewe na wanawe watatu baada ya wiki kadhaa za kujificha nchini Kenya na hatua ya kuondoka kwa hofu iliyotatizwa na vikwazo vya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona. Ajak ameliambia shirika la habari la reuters kwamba maafisa wakuu wa serikali ya Sudan Kusini ambaye alikataa kuwataja, walimuonya kuwa Kiir ametuma kundi la watu kumteka nyara jijini Nairobi.
Ajak amesema magari yaliyokuwa na nambari za usajili wa Sudan Kusini yamekuwa yakimuandama jijini Nairobi ambapo alihamia baada ya takriban miezi 18 ya kutumikia kifungo katika gereza la Sudan Kusini. Alisamehewa mnamo mwezi Januari kutokana na mashtaka kwamba alitatiza amani ya nchi hiyo kwa kuzungumza na vyombo vya habari vya kigeni.
Ajak ataja sababu za kuandamwa
Alipoulizwa sababu ya Kiir kutaka kumuuwa ama kumkamata, Ajak alisema anaamini kuwa rais huyo wa Sudan Kusini alijihisi kutishiwa na juhudi zake za kufichua ufisadi na kuimarisha demokrasia katika nchi hiyo iliyopata uhuru wake mnamo mwaka 2011 na kughubikwa na vita kutoka mwaka 2013- 2018. Ajak alianzisha kundi la viongozi vijana wa Sudan Kusini ambalo limechapisha shtuma dhidi ya uongozi wa Sudan Kusini na kutafuta kuwahimiza vijana kufanya maandamano nchini humo ya kutaka uongozi bora na kutamatishwa kwa ghasia.
Ajak ameihimiza Marekani kuiongezea vikwazo Sudan Kusini ikiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya rais Salva kiir kwa ukatili wake . Ameongeza kuwa nchi hiyo haijawahi kuwa na rais mwengine na Marekani lazima isisitize kuhusu njia ya kufanya uchaguzi ama dunia itakuwa imepoteza mabilioni ya dola kuunda taifa lingine la Afrika lililoporomoka na linaloongozwa na dikteta.Hata hivyo wasemaji wa serikali ya Sudan Kusini Ateny Wek Ateny na Michael Makuei hawakujibu maombi ya kuzungumzia suala hilo.Ajak sasa anapanga kurejelea kazi yake na iwapo atapata nafasi, kukutana na rais Donald Trump kumshukuru kwa shinikizo zilizowekwa na serikali yake dhidi ya Sudan kusini.