Mchungaji aliyepotosha kuhusu corona Uganda ashikiliwa
30 Machi 2020Mchungaji huyo ni miongoni mwa viongozi wa kidini zaidi ya 20 waliokamatwa mwishoni mwa wiki kwa kukiuka maagizo yanayolenga kukabiliana na janga la COVID-19.
Ijapokuwa viongozi wa kidini nchini Ugandawaliazimia kuisadia serikali katika kuhakikisha kuwa maagizo yanayolenga kuepusha kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19 yanatakelezwa, kuna baadhi kama mchungaji Augustine Yiga ambao wanapotosha umma kwa kukanusha madhara ya ugonjwa huo.
Mchungaji huyo ameshtumiwa vikali kwa kuhatarisha maisha ya watu na kukwaza juhudi za kuhamasisha kila mtu ashiriki katika kukabiliana na janga hilo. Viongozi wengine 25 walikamatwa mwishoni mwa wiki kwa kukiuka maagizo ya kuepusha mikusanyiko. Polisi ambayo mwanzoni ilitumia nguvu za kupindukia kukabiliana na wale waliokiuka maagizo inafanya juhudi kuhamasisha watu. Kulingana na msemaji wa polisi eneo la Kampala Patrick Onyango kila mtu ambaye anapotosha umma kuhusu suala ya mrikupo wa COVID-19 atachukuliwa hatua.
Vyombo vya usalama vimeunda jopokazi la pamoja kushirikiana na wafanyakazi wa afya katika kuwafuatilia washukiwa wa ugonjwa huo waliotoroka kutoka karantini.
Miongoni mwa waliokwepa karantini ya siku kumi nan ne ni wanasiasa wakiwemo mawaziri 6 na jamaa zao waliotokea ng'ambo. Kundi hilo limelezewa kuwa tishio kubwa kwa umma huku rais Museveni akiwazuia mawaziri hao kutoshiriki vikao vy baraza la mawaziri. Raia wa kawaida Ibrahim Kakeeto amesema hivi kuhusu vitendo vya watu hao mashuhuri.
Katika habari zingine, hii leo rais Yoweri Museveni wa Uganda na viongozi wenzake wa shirikisho la maendeleo kanda ya pembe ya Afrika IGAD wamefanya mkutano kwa njia ya video kujadili mikakati ya pamoja ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii, Uganda imeripoti kuwa visa 33 vya ugonjwa.
Lubega Emmanuel DW Kampala