1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aahidi kuisadia Uturuki kujiunga na EU

19 Oktoba 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesifu hatua zilizopigwa katika kuisaidia Uturuki kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi, na kuahidi kuisadia katika mchakato wake uliokwama wa kuomba uanachama wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1GqID
Kansela Merkel akiwa na mwenyeji wake rais Recep Tayyip Erdogan mjini Istanbul Oktoba 18.
Kansela Merkel akiwa na mwenyeji wake rais Recep Tayyip Erdogan mjini Istanbul Oktoba 18.Picha: Getty Images/G. Bergmann/Bundesregierung

Merkel alifanya mazungumzo mjini Istanbul na waziri mkuu Ahmet Davutoglu na rais Recep Tayyip Erdogan, wakati wa ziara muhimu ya siku moja, iliyokuja wakati Ujerumani ikiyumbishwa na shambulizi la kisu dhidi ya mwanasiasa anayewaunga mkono wakimbizi.

Merkel alinukuliwa na duru za ujumbe wa Ujerumani katika ziara hiyo, akisema kuwa mazungumzo na rais Erdogan yalikuwa ya maana na ufanisi, na kuongeza kuwa kudhibiti uhamiaji ndilo lililokuwa lengo la mataifa hayo mawili.

Umoja wa Ulaya unaitaka Uturuki iimarishe ulinzi wa mipaka yake na isaidie kudhibiti mmiminiko wa kihistoria wa wakimbizi kutoka Syria na kwingineko, wanaokimbia migogoro, ukandamizaji na umaskini.

Kansela Merkel akiwa na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu kabla ya mkutano wao mjini Istanbul siku ya Jumapili.
Kansela Merkel akiwa na waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu kabla ya mkutano wao mjini Istanbul siku ya Jumapili.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

Kwa upande wake Uturuki inataka itambuliwe zaidi kwa mchango wake wa kuwapokea wakimbizi zaidi ya milioni mbili wa Syria, iongezewe msaada wa kifedha na kuharakisha mchakato wake wa kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Merkel na viongozi wa Uturuki waliashiria kuwa maafisa wamepiga hatua kuelekea makubaliano juu ya ushirikiano, ingawa hakuna aliyesema makubaliano ya mwisho yalikuwa yamefikiwa.

Kansela huyo wa Ujerumani alisema serikali yake mjini Berlin ilikuwa tayari kuunga mkono mazungumzo juu sura ya 17 ya mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya-- ambayo inashughulikia masuala ya kiuchumi na kifedha -- na pia kuzingatia kuanzisha mazungumzo kuhusu sura nyingine 35 za kisera za Umoja wa Ulaya.

"Uturuki na Umoja wa Ulaya wanakubaliana kwamba ushirikiano wa karibu unahitajika kushughulikia matatizo ya wakimbizi," alisema Merkel baada ya mazungumzo na Erdogan, na kuongeza kuwa kuna makubaliano kuhusu kuharakisha maombi ya Uturuki kijuinga na Umoja wa Ulaya na vile vile kulegeza masharti ya viza wa Waturuki wanaotaka kusafri katika kanda ya Schengen, na pia makubaliano ya kuwapokea tena wahamiaji watakaokataliwa.

Erdogan, ambaye kwa miezi kadhaa ameukosoa vikali mtazamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu Uturuki, alisema pia anataka sura zaidi za mchakato wa kijiunga na umoja huo zifunguliwe. Pia aliita Ujerumani na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya kuisadia Uturuki kupambana na ugaidi.

Wakimbizi wakienda kupanda basi la kwenda Austria, baada ya kuvuka mpaka wa Slovenia na Croatia Oktoba 17.
Wakimbizi wakienda kupanda basi la kwenda Austria, baada ya kuvuka mpaka wa Slovenia na Croatia Oktoba 17.Picha: picture alliance/AA/A. Beno

"Nilisisitiza kuwa tunahitaji kuchukuwa hatua za pamoja dhidi ya mashirikaya kigaidi. Tumezungumzia pia kujiunga kwa Uturuki na Umoja wa Ulaya," alisema rais Erdogan.

Davutoglu asifu "mkakati bora"

Awali katika mazungumzo na Merkel, waziri mkuu Ahmet Davutoglu alisifu kile alichokiita mkakati bora wa Umoja wa Ulaya kuwashughulikia watu zaidi ya milioni mbili waliokimbilia Uturuki kutoroka vita vya Syria. Alisema Uturuki ilikuwa imeachwa peke yake na jumuiya ya kimataifa, "lakini sasa tunafurahi kwa sababu kuna mkakati mzuri."

Merkel alisema ukweli kwamba Uturuki imetekeleza jukumu kubwa la kuwahudumia wakimbizi zaidi ya milioni mbili kwa ufadhili mdogo, ulipelekea shinikizo lilisababisha mmiminiko wa sasa wa wakimbizi barani Ulaya. Uturuki imetaka ipatiwe kiasi cha euro bilioni tatu kwa ajili ya kuwahudumia wahamiaji walioko kwenye mipaka yake -- kiasi ambacho ni mara tatu ya kile ambacho umoja huo ulichotangaza kutoa awali.

Zaidi ya wakimbizi 630,000 wamewasili barani Ulaya mwaka huu, wengi wakitumia njia hatari ya kuvuka bahari kutokea Uturuki kwenda Ugiriki. Watu wengine 12 walizama nje ya pwani ya Uturuki siku ya Jumamosi, na Jumapili askari wa pwani wa Ugiriki walisema wahamiaji watano akiwemo mtoto mchanga na wavulana wawili walifariki wakati wakijaribu kuvuka bahari ya Aegean.

PEGIDA yaanza upya harakati zake

Wakati Wajerumani wengi wamewakaribisha wakimbizi, kumekuwepo na upinzani pia, ambapo chama cha Merkel kimepoteza uungwaji mkono, huku vuguvugu la maandamano ya kuupinga Uislamu la PEGIDA, likianza tena kuvutia maeneo ya wafausi.

Vuguvugu hilo linalodai kupinga uhamiaji na kuenezwa kwa Uislamu katika mataifa ya Magharibi, Jumatatu linafanya maandamano yake ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuasisiwa kwake mjini Dresden, katika jimbo la mashariki la Saxony.

Waandamanaji wa PEGIDA wakiwa wamebeba mfano wa mhimili wa kunyongea ukiwa na ujumbe usema imehifadhiwa kwa ajili ya Merkel, na naibu wake Sigmar Gabriel.
Waandamanaji wa PEGIDA wakiwa wamebeba mfano wa mhimili wa kunyongea ukiwa na ujumbe usema imehifadhiwa kwa ajili ya Merkel, na naibu wake Sigmar Gabriel.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Wasiwasi unaozidi kuhusu wakimbizi uliishia katika vurugu mjini Cologne siku ya Jumamosi, wakati mwanaume aliyekuwa na kisu alipomshambulia mgombea wa nafasi ya meya wa jiji hilo Henriette Reker, mwenye umri wa miaka 58, ambaye amekuwa akijihusisha zaidi na kuwasaidia wakimbizi, na kuwajeruhi wengine wanne. Reker alishinda uchaguzi wa Jumapili kwa wingi wa kutosha.

Wakati mmiminiko wawakimbizi ukiendelea, Hungary ilifunga mpaka wake na Croatia, na kuwalaazimu malefu ya wahamiaji kutafuta njia nyingine kwenda Ulaya kaskazini kupitia Slovenia hadi Austria. Lakini wakati idadi ikiongezeka zaidi na zaidi, Slovenia ilisema haiwezi kushughulikia wakimbizi zaidi ya 25,000 wanaowasili kwa siku, uamuzi ambao ulitishia kusababisha mgogogro wa kibinaadamu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae

Mhariri: Josephat Charo