Merkel aanzisha mazungumzo ya kuunda serikali na SPD
7 Januari 2018Chama cha SPD kwa shingo upande kilikubali kufanya mazungumzo ya awali ya uchunguzi na kinajivuta na kuonesha "nyodo" na kwamba mazungumzo hayo hayatakuwa rahisi. Kukivutia chama hicho kushirikiana nacho ni kamari anayocheza Merkel katika kuunda serikali imara na kurefusha uongozi wake wa miaka 12 baada ya juhudi zake kuunda ushirika na vyama viwili vidogo kushindwa mwaka jana.
Chama cha SPD , ambacho kilishiriki kutawala katika kile kinachoitwa "muungano mkuu" pamoja na vyama vya kihafidhina vinavyoongozwa na Merkel kwa miaka minne iliyopita, kimeapa kuingia katika upinzani baada ya kupata matokeo yake mabaya kabisa tangu mwaka 1933 lakini kilitafakari upya msimamo wake huo baada ya rais kuingilia kati.
Upinzani dhidi ya muungano huo katika serikali ni mkubwa katika SPD, kundi linaloitwa "NoGroko" ikiwa na maana "Hapana kwa muungano mkuu", limeundwa miongoni mwa wanachama kufanya kampeni dhidi ya kufanya kazi pamoja na Merkel tena, likisema kwamba hali hiyo itakigharimu chama cha SPD kupoteza kura na kukifanya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD kuwa kiongozi wa upinzani.
"Hatupaswi kufanya mambo yaonekana mazuri kuliko yalivyo, chama cha SPD kina shaka kubwa juu ya kurejewa kwa muungano huo mkubwa," mwanachama mwandamizi wa SPD Manuela Schwesig amesema katika mahojiano na redio ya Ujerumani Deutschlandfunk radio.
Muungano mkuu
Norbert Roemer , kiongozi wa SPD katika bunge la jimbo la North Rhine - Westphalia , aliiambia kampuni ya magazeti ya RND kwamba hakuna wabunge kutoka jimbo lake wanapendelea muungano huo mkuu - tofauti na miaka minne iliyopita, kutokana na uzoefu uliokuwapo hapo kabla ikiwa na maana hawamuamini tena Merkel.
Wazo la muungano mkuu, kwa kawaida ni chaguo la mwisho kwa kuwa linaufanya upinzani kuwa na wabunge wachache, na hilo haliungwi mkono na wengi, ambapo uchunguzi wa maoni kwa ajili ya kituo cha matangazo cha ARD umeonesha zaidi ya nusu ya Wajerumani , asilimia 52 wana shaka wakati asilimia 45 wanapendelea.
Vyama hivyo bila shaka vitapambana kuhusiana na suala la uhamiaji, kodi, matibabu na Ulaya. Volker Bouffier , mwanachama mwandamizi wa chama cha Merkel cha Christian Democratic CDU , ameliambia gazeti la Rheinische Post kuwa chama chake kinakusudia kuunda serikali ya muungano mkuu.
Lakini aliongeza: "Iwapo hilo litafanikiwa bado haijulikani. Haiwezi kutokea kwa gharama yoyote."
Kiongozi wa wabunge wa SPD bungeni Andrea Nahles alionesha ishara ya maridhiano zaidi, akisema hatachora mistari yoyote myekundu kabla ya mazungumzo, akiliambia gazeti la Bild am Sontag, kwamba "Majadiliano yana maana hutapata mafanikio ya asilimia 100 ya madai yako."
Serikali mpya wakati wa Pasaka
Iwapo majadiliano yatakuwa ya mafanikio, serikali mpya huenda ikawepo ifikapo wakati wa sikukuu ya Pasaka, amesema.
Horst Seehofer , kiongozi wa chama cha Christian Social Union CSU chama ndugu na chama cha kansela Merkel cha CDU , amesema ana matumaini vyama vitakubaliana kutawala kwa pamoja, akisema : "Nafikiri tutaweza."
Washirika hao wamekubaliana kutotoa taarifa wakati wa mazungumzo hayo ya matayarisho, ambayo yanatarajiwa kumalizika siku ya Alhamis. Iwapo watapata msimamo wa pamoja wa kutosha na chama cha SPD kinapata uungwaji mkono kutoka kwa wanachama wake katika kura , vyama hivyo vitaendelea na mazungumzo kamili ya kuunda serikali.
Lakini iwapo majadiliano yatashindwa, taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Ulaya huenda likakabiliwa na uchaguzi mpya, ama kwa mara ya kwanza katika enzi za baada ya vita, serikali yenye wingi mdogo bungeni chini ya Merkel itaundwa.
Mazungumzo yaliyoshindwa mwaka jana ya kuunda serikali yalihusisha vyama vya kihafidhina vinavyoongozwa na Merkel , pamoja kile kinachopendelea wafanyabiashara cha Free democrats FDP na chama cha walinzi wa mazingira The Greens.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Caro Robi