Merkel apania kuing'oa AfD bungeni
15 Machi 2018Wakati akianza kutumikia muhula wake wa nne madarakani, Merkel ameweka wazi kwamba analenga kukiondoa pia chama hicho.
Katika mahojiano yake ya kwanza makubwa tangu alipochaguliwa tena siku ya Jumatano , kansela Angela Merkel alisema moja ya lengo lake kuu katika serikali mpya ni kuwavutia wapiga kura kurejea katika kukipigia kura chama chake ambao wamepotelea katika chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD.
"Lengo letu ni kutatua matatizo ya wale wapiga kura waliopiga kura kwa misingi ya upinzani," Merkel alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni ya taifa cha ARD.
"Hii ina maana , bila shaka, nia yake ni kupunguza idadi yao na kuwaondoa kutoka bungeni," aliongeza.
Alisisitiza, hata hivyo, kwamba lengo kuu la serikali yake ni kutatua matatizo yanayowakumba wapiga kura wa Ujerumani.
Merkel apingwa
Merkel alichaguliwa tena kwa muhula wa nne kuwa kansela kwa wingi wa kura tisa tu.
Licha ya kuwa kura ni siri, matokeo yanaashiria kwamba wabunge ndani ya muungano wa serikali yake pamoja na kundi la wahafidhina anaowaongoza pamoja na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SPD walipiga kura kumpinga.
Chama cha Merkel cha Christian Democtaric Union CDU na chama cha SPD vilipata vipigo katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba , vikipoteza wapiga kura kwa chama cha AfD. Chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia kiliingia katika bunge , Bundestag kwa mara ya kwanza baada ya kupata asilimia 12.6 ya kura. Kwa hivi sasa ndio chama kikuu cha upinzani bungeni.
Wanasiasa wa chama cha AfD hususan hawapendelei sera za Merkel kuhusu wakimbizi na mara kadhaa wametoa mwito wa kuondolewa Merkel kutoka madarakani.
Wakati wa upigaji kura bungeni siku ya Jumatano, msaidizi wa mbunge wa chama cha AfD alifukuzwa kutoka katika eneo la watazamaji baada ya kufungua bango ambalo lilikuwa limeandikwa "Merkel lazima aondoke."
Mbunge mwingine wa chama cha AfD alitozwa faini kwa kutuma picha katika mtandao wa kijamii wa Twitter wa kura yake aliyopiga, akionesha kwamba alipiga kura dhidi ya Merkel, pamoja na ujumbe : "Sio kansela wangu." Sheria za bunge zinaeleza kwamba kura ni lazima zibakie kuwa siri.
Mwandishi: Sekione Kitojo / English page
Mhariri: Daniel Gakuba