Merkel asema ataunga mkono Uingereza kujitoa EU
21 Novemba 2018Amesema hayo kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipokuwa akihutubia bunge leo mchana mjini Berlin. Pia ametupilia mbali miito kutoka kwa wabunge wenye siasa kali za mrengo wa kulia kuacha kuunga mkono makubaliano yanayoungwa mkono na Umoja wa mataifa kuhusu uhamiaji.
Waziri mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema jana kwamba serikali yake itapiga kura dhidi ya mswada wa Umoja wa Ulaya kuhusu makubaliano ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo yaani Brexit iwapo maelezo yaliyomo katika mswada huo kuhusu Gibraltar hayatabadilishwa. Gibraltar inatarajiwa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Uingereza ifikapo mwezi Machi, licha ya kuwa asilimia 96 ya wakaazi wake walipiga kura katika kura ya maoni mwaka 2016 nchini Uingereza kubakia katika kundi hilo la mataifa.
"Tunafahamu ni vigumu kiasi gani majadiliano haya yalivyo nchini Uingereza, lakini naweza kusema kwa Ujerumani kwamba tutakubaliana na makubaliano ya kujitoa," Merkel aliwaambia wabunge leo Jumatano wakati wa mjadala wa bajeti.
"Bado tunapingamizi kutoka Uhispania. Siwezi kusema kwa hakika vipi tunaweza kutatua suala hili, lakini nina matumaini litatatuliwa siku ya Jumapili. Katika siku zinazokuja kazi zaidi itafanyika kuhusiana na uhusiano wa hapo baadaye kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya."
Ushirikiano mzuri na Uingereza
Merkel amesema katika hotuba yake kwamba nchi yake inataka kujenga ushirikiano mzuri na Uingereza baada ya Brexit. Katika hotuba yake amesisitiza kwamba yeye pamoja na serikali yake watafanya kila linalowezekana kuhakikisha hilo linawezekana.
Pia Merkel alipuuzia miito kutoka kwa wabunge wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia kwamba Ujerumani iondoe uungaji wake mkono kwa makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji.
Nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Marekani, Hungary, Austria, Israel, Australia na Poland, zimetangaza kwamba hazitaunga mkono Mkataba wa dunia wa uhamiaji salama, utaratibu mzuri na wenye kuratibiwa, ambao umepangwa kuidhinishwa mwezi ujao mjini Marrakech , nchini Morocco.
Upinzani umekuja hususan kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia chama mbadala kwa Ujerumani AfD, lakini wabunge kadhaa kutoka chama cha Merkel pia wameanza kuhoji makubaliano hayo. Merkel amesema.
"Mkataba huu kwa wahamiaji pamoja na wakimbizi ndio jibu sahihi wakati tukiwa mwanzoni mwa kutatua matatizo ya dunia kwa pamoja kimataifa."
Waziri wa afya Jens Spahn ametoa wito hivi karibuni wa mjadala mpana kuhusu mkataba huo, iwapo inahitajika, ucheleweshwe ili kuweza kuufanya bora zaidi.
Akiwasilisha mswada wa bajeti wa serikali yake wa euro bilioni 356 kwa mwaka 2019, Merkel ameelezea mipango ya kuwekeza zaidi katika huduma ya afya kwa watoto na wazee, kuchukua hatua za kuimarisha ujumuisho kwa wahamiaji, kupandisha viwango vya malipo ya uzeeni na kuimarisha nishati endelevu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga