Merkel asema Ujerumani ya sasa ni bora zaidi
7 Septemba 2016Vichwa vya habari katika magazeti na ripoti za televisheni na redio mara tu baada ya CDU kushindwa uchaguzi huo wa Jumapili, zilitazamiwa kumrejesha Kansela Merkel nyuma, na hotuba ya leo ilidhaniwa kuwa ingekuwa nyepesi na laini. Lakini hivyo sivyo ilivyokuwa, kwani kwenye hotuba ya bungeni ya leo Jumatano (7 Septemba 2016), ambapo alionekana kusimama imara.
"Hali yetu leo ni bora zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita kwetu sote. Hapana shaka, bado kuna mambo ya kufanywa. Changamoto kubwa ikiwa kuwarejesha nyumbani wahamiaji ambao hawawezi kubakia hapa na sisi. Na kwa uadilifu kuwahudumia raia wetu, huku tukiwafahamisha kuwa tunapaswa kuwasiaidia wale wenye haki ya kusaidiwa," aliwaambia wabunge.
Katika hotuba hii, ambayo tayari imeshaonesha kuzua mjadala mkali, Kansela Merkel amesema si kweli kuwa mmiminiko wa mamia kwa maelfu ya wakimbizi nchini Ujerumani utapunguza mafao wanayopata raia wazawa wa Ujerumani, hoja ambayo imekuwa ikitumiwa na wapinzani wake wa kisiasa.
Chama chake, CDU, kiliangushwa kwenye uchaguzi wa mwishoni mwa wiki na chama kinachopinga wahamiaji nchini Ujerumani, AfD, katika jimbo la Mecklenburg-Vorpommern, kwa hoja hiyo hiyo dhidi ya wakimbizi.
Wapigakura kwenye jimbo hilo walitumia nafasi hiyo kumuonesha kutokubaliana na sera yake ya kufungua milango kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka mataifa yenye Waislamu wengi, hasa baada ya matukio kadhaa ya mashambulizi kwenye miji ya kusini mwa Ujerumani, lakini kwenye hotuba yake ya leo bungeni, Kansela Merkel amesema ugaidi si jambo linalohusiana moja kwa moja na wakimbizi.
"Licha ya kuwa tulikumbwa na mashambulizi mabaya ya Ansbach na Wurzburg, ugaidi si jambo jipya lililokuja na wakimbizi kwetu. Hata kama si kila mkimbizi anakuja na dhamira njema, hatupaswi kuwahukumu kijumla-jamala. Kuifanya Ujerumani kuwa salama, ni pamoja na kuwaonesha wengine kwamba wanaadamu wenzetu wanaweza kututegemea sisi wanapokuwa na matatizo," alisema Kansela Merkel.
Makubaliano na Uturuki ni sahihi
Sambamba na hilo, alitetea pia namna anavyoliendea suala la mahusiano kati ya nchi yake na Uturuki, akiwakosoa wale wanaomwambia ameshinda kulaani hatua kali za ukandamizaji zinazochukuliwa na utawala wa Rais Tayyip Erdogan baada ya jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa mwezi Julai.
Merkel amesema makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na serikali ya Uturuki yaliyolenga kuzuia mmimiko wa wahamiaji yalikuwa hatua muhimu na inayoweza baadaye kuigizwa kama msingi wa makubaliano na mataifa mengine.
Mdahalo wa jioni ya leo kuhusiana na hotuba hii iliyoshadidia msimamo na muelekeo wa Kansela Merkel kwa masuala ya wakimbizi, usalama, na sera yake ya nje unatazamiwa kuwa mkali sana.
Tayari msuguano ndani ya serikali yake ya muungano umeshadhihirika, huku mshirika wake mkuu, chama cha SPD kikionekana kujipanga kumpiku.
Upinzani mkali pia umo ndani ya chake mwenyewe cha CDU, huku chama ndugu cha CSU kikiwa tangu mwanzoni mbali sana na sera ya wakimbizi ya Kansela Merkel.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf