1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel asisitiza umuhimu wa Umoja wa Ulaya kwa Ujerumani

Sekione Kitojo
22 Februari 2018

Kansela Angela Merkel ameonya kuhusu mbinyo unaoukabili hivi sasa Umoja  wa Ulaya, akianisha majukumu muhimu ya hapo baadaye  ya kundi hilo la mataifa ambalo serikali yake ya muungano utakuwa nalo.

https://p.dw.com/p/2t9Or
Deutschland Regierungserklärung Merkel
Picha: Reuters/A. Schmidt

Ulaya  imo  katika  mbinyo  kisiasa na  kiuchumi duniani  kote, Merkel aliwaambia  wabunge  mjini  Berlin  hii  leo. Ujerumani  inaweza kufanya  vizuri  iwapo Ulaya  inafanya  vizuri, alisema  Merkel  na kuainisha  umuhimu  wa  Umoja  wa  Ulaya  kwa  Ujerumani. Amesema  hayo  leo katika  bunge  la  Ujerumani  Bundestag  kabla ya  kufanyika  mkutano  wa  kilele  wa  Umoja  wa  Ulaya  ambao utashughulikia  bajeti  ya  hapo  baadaye  ya  mataifa  hayo.

Deutschland Bundestag
Bunge la Ujerumani Bundestag likihutubiwa na kansela MerkelPicha: Reuters/A. Schmidt

Merkel  aligusia  pia  mizozo  ya  kikanda  ambapo  alisema  Umoja wa  Ulaya  unapaswa  kuchukua  jukumu  la  juu  kutatua  mizozo  na kudokeza  haja  ya  kutatua mzozo nchini  Syria.

Kwa jumla kuna  mengi ya kufanya katika sera zetu za  mambo ya kigeni. mambo  hayo  ni  kuhusu uhusiano wetu na Urusi, China na pia katika  jukumu  letu la  kutafuta suluhisho  la  mizozo  ya  kikanda. Katika  hali  ya  kutisha  tunayoiona  nchini  Syria , ambapo utawala wa  nchi  hiyo haupambani  na  magaidi, bali na  wananchi  wake , unaharibu mahospitali  na  ni  mauaji  ambayo  tunapaswa  kuchukua jukumu  la  kuyazuwia.

Deutschland Regierungserklärung Merkel
Kansela Angela Merkel akizungumza bungeniPicha: Reuters/A. Schmidt

Kansela  wa  Ujerumani  amesema  kwamba  kujitoa  kwa Uingereza kutoka Umoja  wa  Ulaya  kunatoa fursa  kwa Umoja  huo  kufikiria kwa  upana  mfumo  wake  wa  kifedha. Akihutubia  bunge  la Ujerumani  Bundestga, Merkel  aliweka  wazi  kwamba  hatma  ya Umoja  wa  Ulaya  litakuwa  suala  la  umbele  katika  muhula  wake wa  nne  madarakani, iwapo  makubaliano  ya  kuunda  serikali  ya mseto  baina  kati  ya  wahafidhina anaowangoza na  Wademocrats ambao  wanaunga  mkono  Umoja  wa  Ulaya  utaidhinishwa  na wanachama  wa  chama  hicho  cha  SPD.

Mkutano wa viongozi wa Ulaya

"Tunahitaji mwanzo  mpya  kwa  Ulaya," Merkel  alisema , na kuongeza  kwamba  mjadala  unaokaribia  juu  ya  bajeti  mpya  kwa kundi  hilo  la  mataifa  27  baada  ya  Uingereza  kujitoa mwaka 2019 unaweza  kusababisha  baadhi  ya  mabadiliko  makubwa.

"Mjadala  juu  ya  hali  ya  baadaye  ya  mfumo  wa  kifedha  pia  ni fursa  ya  kuangalia  utaratibu  wa  kifedha  wa  Umoja  wa  Ulaya kwa  jumla" amesema.

Viongozi  katika  mkutano  wa Ijumaa watajadili  iwapo  kuimarisha bajeti  ya  miaka  saba  ijayo  kulipia  sera  za  pamoja  katika usalama, ulinzi  na  uhamiaji  kati  ya  mwaka  2021 hadi 2027.

Syrien FSA Operation Olivenzweig Afrin
Jeshi la serikali ya Syria ambalo kansela amelilaumu kwa kuwauwa raia wakePicha: picture alliance/AA/H. Nasir

Ujerumani , ambayo  ina  uchumi  mkubwa  barani  Ulaya, ni mchangia  mkubwa  na  imesema  iko  tayari  kulipa  zaidi  licha  ya baadhi  ya  nchi , kama Uholanzi , kudai  kuwa  kundi  dogo  la  nchi bila  ya  Uingereza , ina  maana ya  bajeti  ndogo.

Merkel ametaka  kuwahakikishia  wale  miongoni  mwa  kundi  la wahfidhina  ambao  wana shaka  bado  juu  ya  ujumuisho  wa  ndani zaidi katika  Umoja  wa  Ulaya  na  kulipia  masikini, nchi wanachama  ambazo  zimezongwa  na  madeni.

"Mshikamano  hauwezi  kufuata  njia  ya  upande  mmoja,"  amesema Merkel.

"Mkataba  wa  uthabiti  na  na  ukuaji  utabakia  kuwa  dira kwa  ajili ya  Ulaya,"  amesema , na kuongeza , akisisitiza  kwamba  mzigo huo  na  ukaguzi  unapaswa  kwenda  mkono  kwa  mkono kama sehemu  ya  mageuzi  ya  kanda ya  sarafu  ya  euro.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Josephat Charo