1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atetemeka tena lakini asema yuko imara

10 Julai 2019

Kansela Angela Merkel amepuuza wasiwasi uliojitokeza kuhusu afya yake na kusema yuko imara na anaweza kuendelea na majukumu yake bila tatizo.Madaktari wa Ujerumani nao wajizuia kuzungumzia afya ya kiongozi huyo

https://p.dw.com/p/3Lrg0
Deutschland | Finnland | Angela Merkel | Antti Rinne
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameupuuza wasiwasi uliojitokeza nchini kuhusu ktetemeka kwake kwa mara ya tatu katika kipindi cha wiki tatu na kusema yuko vizuri kabisa na ana uwezo wa kufanya majukumu yake. Katika mkutano na waandishi habari akiwa na waziri mkuu wa Finnland Annti Rinne, mjini Berlin, Merkel amesema hakuna haja ya kuwepo wasiwasi na kwamba yuko sawa kabisa. 

Merkel amepuuza shambulio la kutetemeka ambalo ni sawa na lile alilopata katikati ya mwezi Juni wakati akiwa na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akisema kwamba tukio la Jumatano liko katika mchakato wa awamu na kwamba yuko sawa. Katika tukio la mwanzo la kutetemeka kwake Kansela huyo wa Ujerumani alisema kwamba ameishiwa maji mwilini katika siku ambayo ilikuwa na jua kali na akaeleza kwamba alipata nafuu na kuwa sawa baada ya kunywa maji glasi tatu.

Deutschland | Finnland | Angela Merkel | Antti Rinne
Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Finnland Annti RinnePicha: Reuters/H. Hanschke

Lakini siku tisa baadae alitetemeka tena wakati alipokuwa anateuliwa waziri mpya wa Sheria Christine Lambrecht na rais wa nchi Frank-Walter Steinmeier katika makaazi ya rais katika kasri la Bellevue mjini Berlin. Merkel amesema ni wazi bado tatizo lake halijesha lakini yuko kwenye mchakato wa kulikabili. Ingawa alipoulizwa ikiwa umma unapaswa kufahamu kuhusu hali yake ilivyo baada ya tukio la kutetemeka kwa mara ya tatu ambapo limetokea ndani ya wiki chache tu Merkel alijibu kwa tahadhari na kusema:

''Naamini kwamba kauli yangu kuhusu hilo nimeshaitowa,Na nadhani kauli yangu kwamba niko sawa itakubalika''

Kansela Merkel pia bila ya kufafanua kuhusu kile alichokiita mchakato wa awamu  amesema tatizo hilo siku moja litakwisha,ingawa bado hajafikia huko.

Leo Jumatano Kansela alitetemeka wakati wa gwaride la kijeshi la  kumpa heshima waziri mkuu Rinne wa Finnland ingawa mara hii hakutetemeka sana kama ilivyohuhudiwa huko nyuma.Madaktari nchini Ujerumani hawajazungumzia chochote kuhusu afya ya Merkel ambayo inaonekana kama ni suala la mtu binafsi hata kwa viongozi wa nchi. Wanasiasa wa ngazi ya juu nchini Ujerumani hawana madaktari binafsi kama ilivyo kwa mfano wa rais wa Marekani. Kimsingi Kansela Merkel anatibiwa  na madaktari wale wale wanaohusika kuutibu umma wa Ujerumani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sekione Kitojo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW