1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atishia kuzuia kampeni za Uturuki

20 Machi 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameonya kuwa kampeni za wanasiasa wa Uturuki zinaweza kupigwa marufuku Ujerumani, ikiwa Uturuki haitaacha matusi yake ya kuilinganisha serikali yake na utawala wa enzi ya wanazi.

https://p.dw.com/p/2ZZLR
Tunesien Besuch Merkel PK mit Beji Caid Essebsi
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Reuters/Z. Souissi

Hayo Kansela Angela Merkel ameyasema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin, akiwa na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe. Kabla ya kuzungumza chochote kuhusu mkutano wake na mgeni wake, Bi Merkel ameomba kuweka sawa suala linalohusu kauli zinazotolewa na viongozi wa Uturuki, wakiongozwa na rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan.

''Bado nasimama na kauli yangu ya awali, kwamba Uturuki inapaswa kuacha kutulinganisha na wanazi, bila kisingizio chochote. Kwa bahati mbaya hali hiyo haijasimamishwa, hatutaruhusu hali hiyo ya wao kutaka kufikia malengo yao kwa njia yoyote ile, ambayo imewafanya kukiuka miiko yote, ikiwemo kutowaonea huruma wahanga wa mauaji yaliyoamlishwa na wanazi.'' Amesema Kansela Merkel.

Bi Merkel amesisitiza Ujerumani inayo haki ya kuchukuwa hatua zozote zinazostahili, ikiwa ni pamoja na kutazama upya ruhusa ambayo tayari ilikuwa imekwishatolewa kwa wanasiasa wa Uturuki kufanya kampeni nchini Ujerumani.

Shina la mzozo ni mikutano ya kampeni

Rotterdam Verhältnis der Niederlande und der Türkei
Kura ya maoni ya tarehe 16 Aprili inataka mabadiliko ya katiba yatakayomuongezea nguvu Rais ErdoganPicha: DW/K. Brady

Mvutano huu wa sasa kati ya Uturuki na nchi za Ulaya, hususan Ujerumani, unatokana na hatua ya nchi za Ulaya kukataza mikutano ya kampeni ya mawaziri wa Uturuki, ambao wanataka kuwashawishi waturuki waishio Ulaya kupiga kura ya ndio katika kura ya maoni ya tarehe 16 mwezi ujao wa Aprili kuhusu mabadiliko ya katiba. Inaaminika kuwa mabadiliko hayo yatampa nguvu zaidi Rais Recep Tayyip Erdogan.

Mara kwa mara Rais huyo amezituhumu nchi za Ulaya kuwa na mienendo sawa na ya utawala wa wanazi. Hapo jana Rais Erdogan alimtuhumu Kansela Angela kutumia mbinu za wanazi.

Hakuna haja ya majibizano

Awali, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ilikuwa imelaani vikali kauli hiyo ya Rais Erdogan, huku lakini ikiongeza kuwa Ujerumani isingependa kujiingiza katika majibizano ya matusi na uchokozi vinavyofanywa na Uturuki. Msemaji huyo  Martin Schäfer amesema malumbano hayo hayasaidia chochote mbali na kumnufaisha Erdogan katika kampeni yake. Schäfer amesema ingawa Ujerumani ni nchi yenye uvumilivu, uvumilivu huo haumaanishi upumbavu.

Nchi nyingine za Ulaya kama Uholanzi zimeishakwaruzana na Uturuki kuhusu mikutano hiyo. Nchini Ujerumani wanaishi waturuki zaidi ya milioni 1.4 ambao wanayo haki ya kupiga kura nchini mwao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dpae

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman