1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: Hakuna utamaduni mchanganyiko

Admin.WagnerD15 Desemba 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema dhana ya utamaduni mchanganyiko nchini Ujerumai inaendelea kuwa "uongo", na kuwataka wahamiaji kuheshimu maadili na utamaduni na pia kujifunza lugha ya Kijerumani.

https://p.dw.com/p/1HNnj
Deutschland CDU Parteitag Horst Seehofer und Angela Merkel
Kansela Merkel na waziri mkuu wa Bavaria Horst Seehorfer.Picha: Reuters/R. Orlowski

Matamshi ya Merkel yalikuwa sehemu ya hotuba ya dakika 70 aliyoitoa katika mkutano mkuu wa chama tawala cha Christian Democratic Union CDU, uliomalizka Jumanne jioni katika mji wa kusini-magharibi mwa Ujerumani wa Karlsruhe, ambao uligubikwa na mgogoro mkubwa zaidi wa Ulaya wa wikimbizi na mmiminiko wa wahamiaji nchini Ujerumani.

"Wale wanaotoroka vita na ukandamizaji watapata hifadhi kutoka kwetu. Wale wanaopata hifadhi na ulinzi kwetu laazima watii sheria zetu, maadili na utamaduni wetu, na ili waweze kutuelewa, laazima wajifunze lugha ya Kijerumani, alisema kansela Merkel.

Merkel alisema suala muhimu ni ushirikishwaji katika jamii na kuongeza kuwa, "yote haya ndiyo kinyume cha utamaduni mchanganyiko. Ukweli unabakia kuwa utamaduni mchanganyiko hupelekea kuwepo na jamii mbadala na hivyo dhana ya utamaduni mchanganyiko inaendelea kuwa uongo."

Wajumbe wa mkutano mkuu wa CDU wakionyesha kumuunga mkono mwenyekiti wao Angela Merkel kuhusu suala la wakimbizi.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa CDU wakionyesha kumuunga mkono mwenyekiti wao Angela Merkel kuhusu suala la wakimbizi.Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

"Imefeli vibaya"

Zaidi ya miaka mitano iliyopita, Merkel aliuambia mkutano wa vijana wa chama cha CDU kuwa mkakati huu wa kukuza utamaduni mchanganyiko umeshindwa vibaya. Mwezi Oktoba mwaka 2010, Merkel alisema kuwa kuwaruhusu watu wenye historia tofuati za kitamaduni kuishi sambamba bila kuwashirikisha katika jamii ya wenyeji hakujafanikiwa katika taifa hili ambalo ni nyumbani kwa Waislamu milioni nne.

Merkel pia alitoa wito wa kupunguza pakubwa mmiminiko wa wakimbizi nchini Ujerumani, katika kujibu manun'guniko ya baadhi ya wanachama wa chama chake, ambayo yametishia kukigawa chama hicho tawala na kumgharimu uungwaji mkono usiyo kifani.

"Tunataka na tutapunguza idadi ya wakimbizi. Kwa sababu hili ni katika yetu sote. Ni maslahi ya Ujerumani na pia ya Umoja wa Ulaya katika muktadha ya kuwahudumia watu, kuwapa makaazi na pia kuwashirkisha katika jamii. Na pia ni katika maslahi ya wakimbizi wenyewe kwa sababu hakuna anaetaka kuondoka nchini kwake kwa maksudi."

Lakini kupunguza idadi hiyo hakutokana na kufunga mipaka ya kitaifa, na badala yake Merkel anashinikiza suluhisho katika maeneo kama Syria ili kudhibiti mmiminiko huo, na wakati huo, kuongeza msaada kwa maeneo yanayotoa msaada wa kitu nje ya Ulaya.

Horst Seehorfer na Merkel katika mkutano mkuu wa CDU mjini Karlsruhe.
Horst Seehorfer na Merkel katika mkutano mkuu wa CDU mjini Karlsruhe.Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Seehorfer ashikilia msimamo

Wajumbe wengi walitaka kuwepo na kikomo cha idadi ya wakimbizi wanaoruhusiwa kuingia kwa mwaka. Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer, alitoa wito mpya siku ya Jumanne, wa kuwepo na kikomo hicho, akisema hakuna nchi yoyote duniani inayopokea wakimbizi pasipo na kikomo.

Seehorfer, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa chama ndugu na CDU - cha Christina Social Union CSU, kinachotawala katika jimbo lake la Bavaria, ambako ndiko wanakoingilia wakimbizi wengine wanaowasili Ujerumani, alisema anaamini bila kuwepo na kikomo, itakuwa vigumu sana kutatua mgogoro wa wakimbizi.

Licha ya ukosoaji wa wazi dhidi ya Merkel kuhusiana na suala la wakimbizi, Seehorfer amesifu uongozi wa Merkel aliyoutaja kuwa wa daraja la juu kabisaa, na kumuambia mbele ya wajumbe zaidi ya 1000 waliohudhuria mkutano huo, kuwa: "Angela unajua, tunakuunga mkono katika nyanja zote."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe, dpae

Mhariri: Daniel Gakuba