Merkel, Hollande kulihutubia bunge la Ulaya
7 Oktoba 2015Wakati Ujerumani ikiadhimisha robo karne tangu kuungana tena kwa upande wa mashariki na magharibi Oktoba 1990, Kansela wa Ujerumani na rais wa Ufaransa watazungumzia changamoto zinazoukabili Umoja wa Ulaya ambao umebadilika sana tangu watangulizi wao - Helmut Kohl na Fracoise Mitterand, walipofanya mkutano wa aina hiyo katika bunge la Ulaya mjini Strassbourg Novemba 22, 1989.
Spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz, mwanasiasa kutoka chama cha Kisoshalisti SPD cha Ujerumani, amesema ziara ya Markel na Hollande ni ya kihistoria kwa nyakati hizi ngumu kihistoria. Schulz ambaye amekuwa akipigania kuwepo na uhusiano wa karibu zaidi kati ya Paris na Berlin, amesema Umoja wa Ulaya unakabiliwa na changamoto kubwa na unahitaji utashi mkubwa kutoka kwa viongozi wake.
Wakimbizi, Urusi kwenye ajenda
Masuala makuu kwenye ajenda ya mkutano huo yatakuwa pamoja na mgogoro wa wakimbizi wanaotoroka vita nchini Syria, ambao kuwasili kwao kwa mamia ya maelfu katika miezi ya hivi karibuni kumesababisha migawanyiko mibaya miongoni mwa mataifa 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya, na kupelekea kurejeshwa kwa udhibiti wa mipakani barani humo, ambako kuondolewa kwake tangu kufunguliwa kwa kile kinachojulikana kama pazia la chuma, kunasifiwa kama mafanikio makubwa.
Mgogoro na Urusi, kuhusiana na hatua yake ya kunyakuwa sehemu ya ardhi ya Ukraine na sasa kujiingiza kwake kijeshi nchini Syria, pia unausababishia Umoja wa Ulaya changamoto kubwa.
Ufaransa na Ujerumani, ambazo ni wasisi wenza wa Umoja wa Ulaya,pia zinatafuta njia za kuimarisha sarafu ya pamoja ya euro, baada ya miezi kadhaa ya kuibuka upya kwa mgogoro kabla ya kuokolewa kwa mara ya tatu kwa taifa la Ugiriki linalokabiliwa na hatari ya kufilisika.
Maafisa mjini Paris na Berlin wamepunguza matarajio ya kutangazwa mikakati mipya ya kisera wakati wa hotuba za viongozi hao zitakazodumu kwa saa mbili na nusu, akianza Rais Hollande majira ya saa 9 za Ulaya ya Kati. Viongozi hao wawili - kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Ufaransa, na kile cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha Ujerumani, watajibu maswali kutoka kwa viongozi wa miungano ya vyama katika bunge hilo.
National Front, UKIP kuzungumza
Viongozi hao watakaouliza maswali ni pamoja na Marine Le Pen kutoka chama cha Ufaransa kinachopinga uhamiaji cha National Front, ambaye umaarufu wake katika uchunguzi wa maoni ni tishio kwa matarajio ya kuchaguliwa tena kwa Rais Francoise Hollande mwaka 2017, wakati ambapo muhula wa Merkel utafikia kikomo pia.
Kundi jingine lililopangiwa kuzungumza ni lile linaloongozwa na chama cha UK Independence, ambacho kinaishinikiza Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni atakayoitisha Waziri mkuu David Cameron katika kipindi cha miaka ijayo.
Mwaka 1989, wakati Kohl na Mitterand walipozungumza mjini Strassbourg wakati Ulaya ikiwa katika mashaka kuhusiana na kusambaratika kwa nguvu ya Kisovieti katika upande wa Ulaya Mashariki, Umoja wa Ulaya ulikuwa na wanachama 12. Hivi sasa una wanachama 28. Na pale ambapo Ufaransa na Ujerumani zilikuwa zikitazamwa kama ushirika uliyosawazishwa katika uongozi, hivi sasa Ujerumani iliyo kubwa na tajiri zaidi, ndilo taifa lililo na nguvu zaidi.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/Reuters/afp.
Mhariri: Caro Robi