1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Johnson kujadili vikwazo kuepusha Covid-19

Daniel Gakuba
30 Juni 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wanajadili vizuizi vya safari vinavyolenga kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona aina ya Delta ambavyo vina kasi kubwa ya maambukizi.

https://p.dw.com/p/3vpKh
UK G7-Gipfel | Merkel und Johnson in Carbis Bay
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (Picha ya maktaba)Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Kansela Merkel amekuwa akipigia debe mpango wa pamoja wa Umoja wa Ulaya kuhusu usafiri ili kudhibiti aina hiyo ya virusi.

Kwa wakati huu mtu yeyote anayeingia Ujerumani akitokea Uingereza anapaswa kujiweka karantini kwa muda wa wiki mbili, hata kama amepata chanjo ya Covid-19 au vipimo vinaonyesha kuwa hana maambukizi ya ugonjwa huo.

Nchini Urusi Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin amesema anapinga pendekezo lolote la kuweka sheria inayowalazimisha Warusi kuchanjwa dhidi ya virusi vya corona, lakini wakati huo huo amewaasa wale wanaopinga chanjo hiyo kuachana na mawazo yao potofu, wakati Urusi ikipambana na wimbi la tatu la maambukizi ya Covid-19.

Russland Moskau | Fernsehauftritt Vladimir Putin "Direct Line with Vladimir Putin"
Vladimir Putin, Rais wa UrusiPicha: Sergei Savostyanov/AFP

Maambukizi ya corona yazidi kusambaa Urusi

Kauli yake hiyo ameitoa wakati Urusi ikiripoti vifo 669 Jumatano, vilivyotokea katika muda wa saa 24, huku takwimu rasmi za serikali zikionyesha kuwa idadi ya vifo vitokanavyo na janga la Covid-19 imekuwa ya juu zaidi mnamo siku mbili zilizopita.

Maambukizi ya Covid-19 nchini Urusi yalishika kasi katikati mwa mwezi Juni, yakichochewa na virusi aina ya Delta vilivyotambuliwa mara ya kwanza nchini India, na kudorora kwa kampeni ya kutoa chanjo.

Ingawa chanjo dhidi ya Covid-19 inatolewa bure nchini Urusi tangu Desemba iliyopita, ni asilimia 15 ya raia wa Urusi ambao wamepata angalau dozi moja ya chanjo hiyo, hii ikiwa ni kulingana na tovuti ya serikali ya Gogov.

Upinzani dhidi ya chanjo ulimfanya meya wa Moscow Sergei Sobyanin kuwalazimisha wafanyakazi wote wa sekta ya huduma kupokea chanjo, hatua ambayo sasa imefuatwa na wakuu wa mikoa kadhaa nchini Urusi.

Russland Impftourismus in Moskau
Baadhi ya Warusi wanahofu kuwa huenda wakalazimishwa kuchanjwa dhidi ya Covid-19Picha: Sergey Satanowsky/DW

Hofu ya ulazima wa chanjo

Hicho ndicho chanzo cha wasiwasi miongoni mwa Warusi kuwa yumkini kinachofuata ni kumlazimisha kila mtu kuchanjwa, wasiwasi ambao Rais Putin alitaka kuuondoa katika mahojiano yake na wanahabari Jumatano.

Uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa Warusi wengi wanapinga kupewa chanjo zilizotengenezwa nchini mwao, chapa Sputnik V, EpiVac Corona, CoviVac na pia Sputnik Light ambayi dozi moja ya chanjo inatosha. Katika juhudi za kuondoa hofu ya wananchi, Putin mwenyewe amesema amepokea chanjo ya Sputnik V.

Kwenye ngazi ya dunia, hadi sasa watu 3,940,888 wamekwishauawa na Covid-19 tangu kuzuka kwa janga hilo Desemba 2019, ikiwa ni kulingana na takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la AFP.

Wapatao 181,755,350 wamekwishaambukizwa virusi hivyo, lakini wengi wao wamekwishapona japo baadhi yao waliendelea kusumbuliwa na madhara yake kwa wiki na miezi baadaye.

rtr, afp