1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kuhutubia baraza la mawaziri wa Uingereza

2 Julai 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atalihutubia hii leo baraza la mawaziri la Uingereza wakati wa ziara yake nchini humo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa kigeni kufanya hivyo katika muda wa karibu miaka 25.

https://p.dw.com/p/3vvVr
UK G7-Gipfel | Merkel und Johnson in Carbis Bay
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Kansela Angela Merkel wakiwa katika kongamano la G-7Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atalihutubia hii leo baraza la mawaziri la Uingereza wakati wa ziara yake nchini humo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa kigeni kufanya hivyo katika muda wa karibu miaka 25. Merkel pia anatarajiwa kufanya mkutano na Waziri Mkuu Boris Johnson na Malkia Elizabeth wa pili. 

Ziara ya Merkel inaonekana kama nafasi kwa Uingereza kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Ujerumani, ambayo ni miongoni mwa washirika wake wakubwa wa kibiashara baada ya miaka kadhaa ya mkwaruzano kufuatia hatua ya Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya.

Soma zaidi: Merkel ajibu maswali ya wabunge kwa mara ya mwisho

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson atakuwa mwenyeji wa Merkel katika makaazi yake ya Chequers, ambapo miongoni mwa mambo mengine viongozi hao wawili watajadiliana juu ya mipango ya usafiri wakati huu wa janga la ugonjwa wa Covid-19.

Merkel, amekuwa akishinikiza kuwepo kwa vizuizi vikali vya usafiri hasa kwa wasafiri wanaowasili Ujerumani kutoka Uingereza, ambayo inakabiliwa na ongezeko la maambukizo ya aina mpya ya kirusi cha Corona cha Delta kinachosambaa kwa kasi zaidi.

Ujerumani iliweka ulazima wa kukaa karantini kwa siku 14 kwa wafasiri wanaowasili Ujerumani kutokea Uingereza. Vile vile, mjadala mpya umeibuka juu ya iwapo mji wa London unapaswa kuandaa mechi za mwisho za mashindano yanayoendelea ya mataifa ya Ulaya EURO 2020.

Merkel pia anatarajiwa kukutana na Malkia Elizabeth wa Pili katika kasri la Windsor baadaye leo mchana

Deutschland Corona-Pandemie Angela Merkel spricht im Bundestag
Kansela Angela Merkel anatarajiwa kukutana na Malkia Elizabeth Picha: Tobias Schwarz/AFP

Viongozi hao wawili pia wanatarajiwa kujadiliana juu ya masuala kadhaa kuanzia kufanya mkutano wa pamoja wa kila mwaka wa baraza la mawaziri la nchi hizo mbili, kufanya programu za kimataduni na vijana miongoni mwa masuala mengine.

Ofisi ya Waziri Mkuu huyo wa Uingereza imesema Merkel atakuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kulihutubia baraza la mawaziri la Uingereza tangu rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, alipohutubia baraza la mawaziri mwaka 1997 kwa mwaliko wa waziri mkuu wa wakati huo, Tony Blair.

Merkel pia anatarajiwa kukutana na Malkia Elizabeth wa Pili katika kasri la Windsor baadaye leo mchana.

Akizungumza kabla ya ziara hiyo, Johnson amemminia sifa Merkel kwa juhudi zake za kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili wakati wa utawala wake.

Katika taarifa yake, Johnson amesema na hapa namnukuu, "Katika muda wa miaka 16 ya utawala wa Merkel kama Kansela wa Ujerumani, uhusiano kati ya Uingereza na Ujerumani umeimarishwa tena."

Merkel anapanga kuachia ngazi nafasi ya ukansela baada ya uchaguzi wa Septemba 26.