1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Macron

15 Mei 2017

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron anatarajiwa kukutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel leo hii wakati ambapo viongozi hao wawili watakubaliana kuhusu kuimarisha mahusiano baina ya nchi zao

https://p.dw.com/p/2cysN
Deutschland Frankreich Merkel und Macron Kombobild
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz/J.-F. Monier

Aidha Macro anataraji kuweka wazi mpango wake kuhusu mustakabali wa Bara la Ulaya. 

Ziara ya Macron nchini Ujerumani inatarajiwa kuanza leo hii majira ya mchana kwa gwaride la heshima kwenye Ofisi za Kansela zilizopo mjini Berlin na hii ni ziara yake ya kwanza ya nje ya nchi tangu kaupishwa kwake kama kiongozi mpya wa Ufaransa mnamo siku ya Jumapili.

Ufaransa na Ujerumani yamekuwa yakichukuliwa kama mataifa muhimu katika Umoja wa Ulaya, na Macron ambaye ni mtetezi wa Umoja huo, tayari ameonyesha nia ya kufanyia kazi ahadi zake za wakati wa kampeni za kuufanyia maboresho na kuuimarisha Umoja huo. Merkel tayari ameunga mkono mwito wa Macron wa kutaka kuwepo kwa mpango mpya wa uwekezaji ndani ya jumuiya hiyo ili kuongeza kasi ya ukuaji.

Merkel pia ameeleza kuheshimu majukumu mazito yanayomkabili kiongozi huyo mdogo mwenye umri wa miaka 39, wakati ambapo anataka kuimarisha uchumi na kukabiliana na hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini mwake. 

Mkutano baina ya Merkel na Macron unakuja wakati ambapo, Macron anatarajia kumtaja waziri mkuu, ikiwa ni siku yake ya kwanza ya kuanza kazi rasmi kama rais. 

Frankreich Paris Amtseinführung Emmanuel Macron
Emmanuel Macron akiwapungia wafaransa baada ya kuapishwa kwenye viwanja vya ElyseesPicha: Getty Images/AFP/C. Triballeau

Chaguo lake linaangukia kwa mwanasiasa wa siasa za wastani za mrengo wa kulia Eduardo Philippe anayetokea chama cha Republican. Chaguo hilo linaibua ishara ya wazi kwamba Macron anataraji kuwavutia vijana wengine wa Republican kujiunga na chama chake kipya cha siasa za mrengo wa wastani cha La Republique en Marche(Republic on the Move, REM) ambacho kitashiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa wabunge mwezi Juni.     

Macron ambaye liwahi kuwa waziri wa masuala ya uchumi katika serikali iliyoondoka madarakani ya siasa za kijamaa iliyoongozwa na Rais Francois Hollande, tayari amewavutia wabunge wengi wa kutoka chama cha siasa za wastani za mrengo kushoto katika hatua zake za mageuzi kwenye siasa za nchini humo. 

Hata hivyo anakabiliwa na mtihani mkubwa wa kupata ushindi wa moja kwa moja wa wingi wa viti bungeni na bila ya hivyo hataweza kufanikiwa kutia msukumo wa kupitishwa kwa mipango yake ya mageuzi kwenye sekta za kazi, mafao, ukosefu wa ajira na elimu. 

Philippe ni meya wa mji wa bandari ya kaskazini wa Le Havre na mbunge wa eneo hilo tangu mwaka 2012. Alisoma vyuo vikuu sawa na Macron na anakubaliana na mengi ya maoni yake kuhusu masuala ya uchumi na kijamii.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Iddi Ssessanga