1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Macron, wahimiza mpango madhubuti kuokoa uchumi

Sylvia Mwehozi
30 Juni 2020

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamehimiza juu ya mpango wa ufufuaji uchumi ulio na nguvu na madhubuti kwa ajili ya Umoja wa Ulaya, wakitaka mpango huo ujadiliwe mwezi ujao. 

https://p.dw.com/p/3eXox
Pressekonferenz Merkel und Macron
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Viongozi hao wamekutana kwa mazungumzo mjini Meseberg, siku chache kabla ya Ujerumani kuchukua urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, mnamo wakati uchumi wake ukikabiliwa na hali ngumu tangu vita ya pili ya dunia. Kwa Ujerumani kuchukua  kiti cha urais wa jumuiya hiyo ya wanachama 27, itakuwa mwisho kwa Merkel akiwa kama Kansela, na huenda jukumu hilo likaamua urithi wa kiongozi huyo aliyepachikwa jina la "Kansela wa Milele".

Kansela Merkel amesema Berlin na Paris zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuunda mwelekeo sahihi kuhusu mustakabali wa baadae wa muungano huo.

"Ujerumani itachukua urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya kuanzia Julai mosi na ninafurahi kwamba tuna uelewa wa pamoja wa kushughulikia changamoto hizi  sote na kwamba tunasaidiana. Matarajio ni makubwa, na tunajua endapo Ujerumani na Ufaransa zitaungana, Ulaya sio lazima iungane. lakini kama ujerumani na ufaransa ziko katika hali mbaya, basi umoja wa ulaya utakuwa sio mzuri," alisema Merkel.

Deutschland Treffen Merkel und Macron im Schloss Meseberg
Merkel akisalimiana kwa mbali na Macron kuzingatia tahadhari ya coronaPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Katika mazungumzo yao, viongozi wote wawili wameunga mkono pendekezo la rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wa euro bilioni 750 kama fungu la kuokoa uchumi wa mataifa yaliyoathirika zaidi bila ya masharti ya kuzirejesha. Nchi za Ulaya ya kusini zinaunga mkono mpango huo wa ufufuaji uchumi, ingawa kundi la nchi nne za Austria, Denmark, Uholanzi na Sweden zinapinga msaada mkubwa wa fedha bila ya masharti.

Rais Macron kwa upande wake amelionya kundi la nchi hizo nne akisema linapinga maslahi yake binafsi, na kwamba haikuwa katika maslahi yao kushuhusia baadhi ya wanachama hususan walioko katika soko muhimu katika uchumi wa Ulaya wakiathirika.

Rais  Macron amesisitiza kuwa "na hiki ndicho tumekuwa tukizungumzia na tutakachofanya kwa pamoja, jinsi gani ya kufanya makubaliano ya Ujerumani na Ufaransa kuwa mafanikio ya Umoja wa Ulaya, ulaya yenye mshikamano, uhuru. Kwanza na rais Charles Michel na rais Ursula Von der Leyen na washirika wetu wote, tunataka kila kitu kifanyike na mpango ukubaliwe mwezi Julai".

Ujerumani inachukua urais wa Umoja wa Ulaya ikiwa na nguvu hasa kutokana na namna ilivyoshughulikia dharura ya kiafya ya janga la kirusi cha corona ukilinganisha na mataifa mengine.

Vyanzo: dpa/afp