Merkel na Macron wasisitiza utandawazi Davos
25 Januari 2018Gazeti la Frankfurter Rundschau kuhusiana na hotuba za kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika kongamano la kiuchumi la Davos linaandika:
"Haishangazi, lakini ni muhimu. Wakati kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron walichozungumza katika kongamano la kiuchumi mjini Davos, kuhusu umuhimu wa dunia kufanyakazi kwa pamoja, na anayekusudiwa kuelezwa hayo hakuwapo katika ukumbi wa mkutano. Ni rais wa Marekani Donald Trump, anayetaka kujitenga, na kuudhoofisha ushirikiano na maridhiano. Trump atahutubia kesho Ijumaa mjini Davos. Matarajio ni kwamba atatetea sera zake za Marekani kwanza, kinyume na wanavyotaka Merkel na Macron. Viongozi hao muhimu katika bara la Ulaya wanatoa ishara kwamba bara hilo lina uwezo wa kupambana licha ya Marekani kutangaza vita vya biashara. Tatizo lakini, kwa Merkel na Macron ni muda , mhariri anaandika. Kwamba ni miezi michache mno imebakia , kwa Ulaya kuweza kuonesha ushindani. Baada ya hapo mataifa wanachama yatakuwa wanaangalia zaidi kuhusu uchaguzi wa mwaka 2019 na kwa hiyo hali hiyo itadhoofika. Trump kwa upande wake muda anao."
Gazeti la Frankfuter Allgemeine, kuhusu mada hiyo ya hotuba ya Merkel katika kongamano la Davos linaandika:
"Ni sahihi kabisa kwa Angela Merkel kutetea utaratibu wa kuendelea kuwa na uhuru katika dunia dhidi ya wakosoaji wake na wale wasiotaka kumpa sifa yake. Kwa sababu utaratibu huu uko kwa maslahi ya kisiasa , kiuchumi na kimkakati kwa Ujerumani. Lakini pia Merkel hana budi kuchukua hatua za kufanyakazi pamoja na makundi dhaifu ya kimataifa , ili kuweza kuondoa hali ya mtengano ,siasa za uzalendo na siasa kali za mrengo wa kulia katika mataifa ya magharibi. Ili kutoleta tena hali ya mivutano kuhusu utandawazi, kutovuruga utaratibu wa kidigitali, na pia uhamiaji. Katika kongamano la Davos mtu anatarajia kusikia ulinzi wa faida za utandawazi, na kuzuwia kurejea nyuma na kutumbukia katika siasa za kizalendo."
Kuhusiana na hatua ya Uturuki kuwashambulia Wakurdi nchini Syria , gazeti la Münchener Merkurs linaandika:
"Hivi sasa kuna mtafaruku mkubwa. Hususan kwa kuwa nchini Syria jeshi la Uturuki likiwa na vifaru vilivyotengenezwa nchini Ujerumani linapambana na Wakurdi. Kuna madai kwamba ni lazima kuzuwia mauzo yote ya silaha kwa sasa. Hii inapendeza masikioni , na ni sahihi, lakini kimsingi ni hatua kubwa zaidi. Hata kama haipendezi. Ulinzi wa nchi yoyote ni suala muhimu sana kwa kila serikali. Kwa hiyo ni lazima kwa kila nchi kujihusisha na nyingine na kuipatia silaha za kutosha. Kwa hilo tunapaswa kuwa pamoja na mwanachama wa NATO Uturuki. Na kwa wakurdi kuwapa silaha kwa ajili ya mapambano yao muhimu dhidi ya IS. Hali hii inaonesha, ni ugumu kiasi gani kutoa jibu muafaka."
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga