Merkel na Seehofer waafikiana kuhusu uhamiaji
2 Julai 2018Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na waziri wake wa mambo ya ndani, Horst Seehofer, wamekubaliana dakika ya mwisho na kuondosha tofauti zao kuhusiana na mvutano juu ya sera ya uhamiaji. Hatua hiyo inaashiria serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Merkel inabaki kuwa imara, kinyume na hofu iliyokuwepo kwamba ingevunjika.
Kansela Merkel amesema Ujerumani itawazuia wahamiaji waliosajiliwa katika nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya kwenye vituo maalumu, huku ikiwa katika mchakato wa kutafuta njia za kuiwarejesha makwao. Merkel amesifu makubaliano yaliyoafikiwa na washirika wake wa Bavaria ambao walikuwa wametishia kujiondoa kutoka serikali yake ya mseto.
Alisema muafaka kati ya chama cha Christian Social Union, CSU, na Christian Democratic Union, CDU, utasaidia kulinda kanuni ya uhuru wa watu kutembea katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya huku ukiiruhusu Ujerumani kuchukua hatua katika ngazi ya kitaifa kupunguza na kudhibiti idadi ya wakimbizi wanaowasili.
"Tunataka kwa upande mmoja kujenga vituo vya muda vya wahamiaji Ujerumani na kuanzia hapo tuwarejeshe makwao chini ya makubaliano na nchi wanakotokea waomba hifadhi na ambako tayari wamesajiliwa," Merkel aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu.
Mwandishi: Josephat Charo/dpae/afpe/rtre