Merkel: Tuko kwenye hatua za mwanzo za kupambana na COVID-19
23 Aprili 2020Akilihutubia bunge leo mjini Berlin, Merkel amesema janga la virusi vya corona liko mwanzoni hivyo Ujerumani bado iko kwenye hatua za awali za kukabiliana na janga hilo.
Amebainisha kuwa Wajerumani hawaishi katika awamu ya mwisho ya janga, kwani ndiyo kwanza wako mwanzoni na hawawezi kurejea kwenye maisha ya kawaida kama ya kabla ya janga kutokea, hivyo maisha yao ya kila siku yatakuwa tofauti.
Amesema ana wasiwasi kwamba Wajerumani wanaanza kupunguza kuzingatia juhudi zilizowekwa za utaratibu wa watu kutokaribiana baada ya serikali ya shirikisho na serikali za majimbo kukubaliana kuanza kufungua maduka wiki hii.
Ujerumani inashika nafasi ya tano katika orodha ya nchi zenye maambukizi makubwa ya COVID-19 ikiwa nyuma ya Marekani, Uhispania, Italia na Ufaransa, lakini idadi ya vifo iko chini kutokana na kuanza mapema kuwapima watu.
Idadi ya wanaopona Ujerumani ni kubwa kuliko visa vipya
Kwa mujibu wa Taasisi ya Afya ya Ujerumani, Robert Koch, Ujerumani ina visa 148,046 vya corona na idadi ya wagonjwa wanaopona ni kubwa kuliko ile ya maambukizi mapya.
Merkel amesema janga la COVID-19 litachukua muda mrefu na kwamba kuamua kuhusu kuweka masharti ya kudhibiti shughuli za kijamii kilikuwa ni kipindi kigumu sana katika uongozi wake kama kansela.
Wakati huo huo, Kansela Merkel ametoa wito wa kuwepo kwa bajeti kubwa ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kusaidia kuufufua uchumi wa umoja huo. Amesema Ujerumani imejiandaa kulipa michango mikubwa katika Umoja wa Ulaya kwa lengo la kuusaidia umoja huo kuondokana na mzozo wa virusi vya corona.
''Tunapaswa kujiandaa, kwa kuonyesha roho ya mshikamano, kutoa michango mikubwa katika bajeti ya Umoja wa Ulaya kwa kipindi kifupi, kuupigia jeki bajeti ya Umoja wa Ulaya kwa sababu tunataka nchi zote wanachama wa umoja huo ziweze kujikarabati kiuchumi,'' alifafanua Merkel.
Merkel ameelezea utayari wake wa kuanzishwa mpango wa pamoja wa kuufufua uchumi kwa miaka miwili ijayo, ili Umoja wa Ulaya uweze kujitegemea tena.
Hata hivyo, ameonya kwamba viongozi wa Umoja wa Ulaya bado hawawezi kuanza kuzungumzia maelezo ya mpango kama huo, licha ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika baadaye leo kwa njia ya video.
Ama kwa upande mwingine Merkel amezungumzia uamuzi wa kuzipunguzia madeni nchi masikini zikiwemo zile za Afrika ili ziweze kupambana na janga la virusi vya corona.
(AFP, DPA, Reuters)