Merkel: Uchaguzi mpya itakwua ni 'makosa'
26 Novemba 2017Kansela Angela Merkel ameibadilisha kauli yake ya awali kuhusu uchaguzi mpya akisema ni "makosa" kuwataka Wajerumani wapige kura tena. Akizungumza katika mkutano wa chama chake cha Christian Democratic Union – CDU katika jimbo la Mecklenburg-Lower Pomerania, Merkel aliongeza kuwa Ujerumani lazima iwe na serikali imara lakini ambayo pia inaisogeza nchi mbele.
Merkel alikuwa akizungumza katika wakati ambapo Ujerumani inashuhudia matukio makubwa ya kisiasa kuwahi kutokea katika miaka mingi – kuvunjika kwa mazungumzo ya awali ya kuunda serikali ya muungano kati ya CDU na chama ndugu cha Bavaria Christian Social Union – CSU, chama cha Kijani cha walinzi wa mazingira na chama kinachounga mkono biashara Free Democratic – FDP wiki iliyopita.
Baada ya kupata matokeo mabaya kabisa katika uchaguzi mkuu wa Septemba, na kukataa kwa chama cha Social Democratic – SPD kujiunga na serikali ya muungano, Merkel aliviomba vyama viwili vidogo vimsaidie kuunda serikali ya walio wengi.
Hata hivyo, baada ya FDP kujiondoa katika mazungumzo ya awali kikitaja tofauti za kinadharia, kiongozi huyo wa muda mrefu wa Ujerumani ameachwa akitafuta suluhisho baada ya miezi miwili bila serikali mpya. Kutokana na hali hiyo, wiki iliyopita Merkel alidokeza kuwa yuko tayari kwa uchaguzi mpya badala ya kuunda serikali ya walio wachache.
Merkel airekebisha kauli yake
Merkel alionekana kuirekebisha kauli yake siku ya Jumamosi, hata hivyo, akiwaambia wanachama wa CDU katika jimbo lake la nyumbani kuwa "kama hatuwezi kufanya lolote na matokeo ya uchaguzi, hatuwezi kuwaomba watu wapige kura tena".
Labda matumaini ya Merkel kuwa serikali ya muungano huenda inaweza kuundwa kutokana na uchaguzi wa Septemba yanasababishwa na chama cha SPD kubadilisha msimamo.
Baada ya miaka minne ya kuongoza pamoja na CDU na kupata matokeo mabaya zaidi kuwahi kutokea katika uchaguzi mkuu, SPD kilitangaza kuwa hakingejiunga na serikali nyingine ya muungano na kingependelea kuwa sauti ya upinzani katika Bundestag.
Hata hivyo, wakati hali ikiendelea kuwa ngumu nao wapiga kura wakikosa amani na kushindwa kuchukuliwa hatua mjini Berlin, SPD kimedokeza kuwa huenda kikabakia madarakani.
SPD yatathmini serikali ya muungano
Siku ya Ijumaa, kiongozi wa SPD Martin Schulz aliitisha uamuzi wa mashinani kuhusu kama chama hicho kinataka kujiunga na serikali la. Kiongozi wa SPD bungeni Andrea Nahles, aliitisha uungwaji mkono Zaidi kutoka kwa tawi la vijana wa chama hicho, ambalo limeelezea wasiwasi kuhusu kujiunga katika serikali nyingine ya mseto.
Lakini Ujerumani huenda ikasubiri kwa muda zaidi ili kupata serikali mpya – Jumamosi, naibu kiongozi wa SPD Thorsten Schärfer-Gümbel alisema hakuna uamuzi wa kujiunga na serikali ya pili ya muungano utakaofanywa kabla ya mkutano wa kitaifa wa chama hicho wa Desemba 7 hadi 9.
Merkel, kwa upande wake, aliyakaribisha mazungumzo yanayopangwa na Schulz na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier wiki hii kujadili uwezekano wa kuungana tena serikalini.
Mwandishi: Bruce Amani/DW/DPA
Mhariri: Yusra Buwayhid