Merkel yaitolea wito Ulaya kupambana na ugaidi eneo la Sahel
2 Mei 2019Kansela Merkel ameyasema hayo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tatu katika eneo hilo la Sahel, ambapo jana aliwasili nchini Burkina Faso, na pia atazitembelea Mali na Niger.
Ni jukumu ambalo Ulaya inapaswa kuchukua , amesema hayo jana Jumatano baada ya kukutana na viongozi wa kile kinachojulikana kama mataifa ya G5 ya Afrika Magharibi mjini Ouagadougou. Iwapo hali ya machafuko itafanikiwa katika eneo hili, kile tunachotaka kukizuwia , kinaweza kuwa katika kiwango kingine," ameonya kansela Merkel. Rais wa Burkina Faso Roch Marc Kabore, ametaka kuchukuliwe hatua za kutatua suala la mzozo wa Libya, ambapo amesema vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo vinaathiri eneo lote la Afrika magharibi. Tatizo hilo ni lazima lipatiwe suluhisho, amesema na kuongeza kwamba bila hivyo haitawezekana kupiga hatua.
Ugaidi ni tatizo la kimataifa
Mapambano dhidi ya ugaidi ni suala la kimataifa, amesema Merkel jana baada ya kukutana na viongozi wa mataifa ya Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger na Chad katika mji mkuu wa Burkina Faso , Ouagadougou. Hili sio jukumu la mataifa haya matano tu, amesisitiza Merkel , bali ni jukumu pia la mataifa ya Ulaya.
"Marais wameeleza vizuri kwamba mapambano dhidi ya ugaidi ni jukumu la kimataifa. Ndio sababu naelewa matakwa ya kuwa na mamlaka ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ujumbe wa mataifa haya matano ya G5 kama ilivyofanywa kwa ujumbe wa UNMISMA lakini kwa mamlaka dhabiti zaidi."
Sekta ya maendeleo yaathirika
Sababu ya tahadhari hii ni kutokana na mashambulizi yanayozidi ya wanamgambo wa Kiislamu sio tu nchini Mali, lakini hata Niger na Burkina Faso. Hali hiyo tete inaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi hizi, kwa kuwa katika mpaka kati ya Mali na Burkina Faso kutokana na mashambulzi haya yanayofanywa na wanagmabo wa Kiislamu mamia ya shule zimelazimika kufungwa. Bibi Merkel ameongeza.
"Sisi katika bara la Ulaya tunahitaji kuchukua hatua zaidi, tunahitaji kuchukua hatua haraka. Baadhi ya mambo tayari yameanzishwa lakini baadhi bado hayajaweza kufanyika, ndio sababu nitachukua hatua za dhati kuona mambo hayo yanatokea haraka na yanatekelezwa haraka kwasababu tunapaswa kuaminika na changamoto ni kubwa."
Tatizo lingine ni kwamba Marekani inajaribu kuzuwia kupatikana mamlaka ya vikosi vya mataifa ya sahel katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ujerumani itazipatia nchi hizo za Sahel kiasi ya euro milioni 60 kwa ajili ya jeshi hilo la pamoja.
rtre, afpe