Mfalme Charles III ajizuwia kuwaomba radhi Wakenya
1 Novemba 2023Siku ya Jumatano (Novemba 1), ziara ya Mfalme Charles III iliingia siku yake ya pili nchini Kenya, ambako aliyatembelea makaburi ya kihistoria ya Kariakor na kuhutubi katika ofisi kuu za Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, huku Camilla akilitembelea Shirika la Kuwalinda Wanyama (KSPCA).
Usiku wa kuamkia Jumatano, Charles na Camilla walikuwa wageni wa Rais William Ruto kwenye chakula cha jioni katika Ikulu ya Nairobi, ambapo mfalme huyo wa Uingereza alielezea jinsi Kenya ilivyo na nafasi muhimu katika maisha yake.
Mfalme Charles alisema anasikitika kwa madhila yaliyowafika Wakenya wakati wa kupigania uhuru na kuyataja matendo hayo kuwa ya kukirihisha na yasiyokuwa na haki.
Soma zaidi: Wapiganiaji uhuru Kenya wamtaka Mfalme Charles III kuomba radhi
Chini ya utawala wa mama yake, Malkia Elizabeth II, serikali ya Uingereza iliendesha kampeni kali na ya kikatili dhidi ya wapiganiaji uhuru wa vuguvugu la Mau Mau, ambapo maelfu waliuawa, kujeruhiwa na kufukuzwa kwenye maeneo yao.
Ijapokuwa hakuomba radhi moja kwa moja, Mfalme Charles alikiri kuwa hicho kilikuwa kipindi kilicholeta machungu na akaonesha nia ya kutaka kukutana na baadhi ya makundi ya walioathiriwa.
Ruto asema yashayopita si ndwele
Kwa upande wake, Rais Ruto alisisitiza kuwa yaliyopita si ndwele, lakini "ili kuyaganga yajayo ipo haja ya kujifunza kutoka kipindi hicho na kuimarisha uhusiano kwa manufaa ya wote."
Ujio wa kiongozi huyo wa Uingereza uliwaleta pamoja Rais Ruto na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, aliyehudhuria karamu hiyo ya usiku.
Soma zaidi: Mfalme Charles III ziarani Kenya
Tume ya haki Kenya yamtaka Mfalme Charles aombe msamaha
Ziara ya Mfalme Charles III imegubikwa na kiwingu cha manung’uniko na kilio cha wahanga wa madhila ya ukoloni kutaka fidia kwa misingi ya sera zilizounda Umoja wa Mataifa.
Wapiganaji wa Mau Mau, waliotambuliwa rasmi mwaka 2003 kama mashujaa, waliadhibiwa sana wakati wa kipindi cha kuwania uhuru, ambapo zaidi ya wapiganaji 10,000 wanaripotiwa kuuawa na kuteswa na wakoloni katika miaka ya 1950.
Miongoni mwa makundi ya wapiganaji ni jamii ya Talai ya Nandi ambapo wamekuwa wakidai fidia kutoka serikali ya Uingereza.
Ziara ya siku nne ya Mfalme Charles III na mkewe Camilla ilitazamiwa pia kuwafikisha hadi mji wa pwani wa Mombasa.
Imetayarishwa na Thelma Mwadzaya/DW Nairobi