1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfuko kwa ajili ya chanjo barani Afrika wazinduliwa

20 Juni 2024

Mfuko wa kiasi cha dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kutengeneza chanjo barani Afrika kimetangazwa na viongozi wa dunia na asasi za afya na kampuni za dawa kwenye mkutano unaofanyika mjini Paris.

https://p.dw.com/p/4hJsZ
Chanjo Afrika
Mfuko wa kiasi cha dola bilioni 1.2 kwa ajili ya kutengeneza chanjo barani Afrika umezinduliwaPicha: Nick Potts/PA Wire/empics/picture alliance

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema kampuni ya kutengeneza chanjo ya Afrika "Accelerator” itakuwa sehemu muhimu ya soko halisi la chanjo barani Afrika. Robo tatu ya fedha hizo zitatolewa na bara la Ulaya.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema kwa njia ya video kwamba nchi yake itachangia dola mlioni 318 kwenye mfuko huo. Ufaransa nayo itatoa dola milioni 100.

Soma pia: WHO yatahadharisha juu ya uhaba wa chanjo ya kipindupindu

Wachangiaji wengine ni Marekani, Canada, Norway na wakfu wa Bill Gates. Lengo ni kupambana na milipuko ya maradhi yanayoongezeka kama vile kipindupindu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat amesema mpango huo utakuwa chachu ya kuendeleza sekta ya dawa na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama.

Amesema mpaka sasa bara la Afrika bado linaagiza asilimia 99 ya chanjo kutoka nje kwa bei kubwa. Mkutano huo wa mjini Paris unahudhuriwa pia na viongozi kutoka Afrika, mawaziri na wawakilishi wa kampuni za dawa.