Mfumo wa refarii msaidizi wa video waigawa Bundesliga
6 Novemba 2017Shirikisho la kandanda Ujerumani – DFB linakabiliwa na shinikizo kuhusu matumizi ya marefarii wasaidizi wa video maana kila wiki yanafanyika maamuzi yenye utata. Kuanzishwa kwa mfumo wa video, unaofuatiliwa na marefarii mjini Cologne ili kurekebisha makosa yanayofanywa na marefarii wa uwanjani kote nchini, kwa majaribio ya mwaka mmoja, kulikaribishwa kwa matumaini makubwa mwanzoni mwa msimu huu.
Lakini baada ya miezi mitatu tu, matumizi yasiyokuwa thabiti ya mfumo huo na ukosefu wa uwazi kuhusu matumizi yake vimezusha mashaka miongoni mwa vilabu vya Bundesliga. Awali ilisemekana kuwa refarii wa vodeo angeingilia kati tu kama refarii wa uwanjani angefanya kosa kubwa – linalohusu vitu vinavyoweza kuubadilisha mchezo kama vile mabao, mikwaju ya penalty na kadi nyekundu.
Hata hivyo, baada ya mechi tano za kwanza kuchezwa msimu huu, hoja hii ililelegezwa bila vilabu kuarifiwa n ahata rais wa DFB Reinhard Grindel alipigwa na butwaa. Huku maamuzi Zaidi yakichambuliwa, mamlaka ya refarii uwanjani yanatiliwa shaka, ijapokuwa Grindel anasisitiza kuwa uamuzi kawaida huwa ni wa refarii aliyeko uwanjani
Afisa mkuu mtendaji wa Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke anaunga mkono matumizi ya video lakini ametoa wito wa kuwapo na uthabiti. Amesema hatua inapaswa kuchukuliwa haraka na kuwa kipindi kinachoanza cha mechi za kimataifa kinapaswa kutoa fursa kwa DFB kuitathimini teknolojia hiyo.
Kocha wa Augsburg Stefan Reuter anasema ni muhimu wadau wote wakae meza moja. Anaunga mkono video lakini anasema mazungumzo ya kila wiki kutokana na utata unaojitokeza sio mazuri.
Naye rais wa klabu ya Freiburg Fritz Keller anasema mfumo huo unapaswa tu kufutiliwa mbali na waache mpira uchezwe tu na maamumizi kutolewa uwanjani papo hapo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman