Mgahawa wa kiyahudi washambuliwa Ujerumani
8 Septemba 2018Watu waliojifunika nyuso zao waliushambulia kwa mawe na chupa mgahawa mmoja wa chakula wa kiyahudi na kumjeruhi mmiliki wa mgahawa huo katika kile kinachosadikika kuwa shambulizi linalohusiana na chuki dhidi ya wageni ambalo limetokea pembezoni mwa wimbi la maandamano makubwa ya wanazi mambo leo katika mji wa Mashariki mwa Ujerumani.
Taarifa hizi zimetolewa na maafisa pamoja na kutangazwa katika taarifa leo jumamosi. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya mkoa wa Mashariki mwa Ujerumani amesema kitendo hicho kilichochochewa kisiasa na ambacho kina misingi ya chuki dhidi ya wageni ni kibaya zaidi kuwahi kufanywa kuelekea shambulizi la Chemnitz la mwezi uliopita.
Mji huo umekumbwa na vurugu na ghasia za matumizi ya nguvu yanayofanywa na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia,sambamba na maandamano ya kupinga wageni tangu lilipotokea tukio la kuuwawa kwa kuchomwa kisu mwanamme mmoja wa Kijerumani,shambulio ambalo linasemekana kufanywa na wakimbizi wanaoomba hifadhi.
Polisi ya jimbo la Saxony imethibitisha kupokea malalamiko juu ya kushambuliwa kwa mgahawa wa Shalom. Watu kadhaa waliovaa mavazi meusi na kujifunika nyuso zao waliokuwa wamebeba mawe,chupa na nondo waliiushambulia mgahawa huo Agosti 27 na mmiliki wa Mgahawa huo Uwe Dziuballa akajeruhiwa kwenye bega. Mgahawa huo uliofunguliwa mwaka 2000 umewahi kushambuliwa mara kadhaa siku za nyuma.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFP/DPA
Mhariri:Zainab Aziz