Mgawanyiko wa jeshi kuharakisha utawala wa kiraia Myanmar
1 Aprili 2008Mgawanyiko ndani ya utawala wa kijeshi nchini Myanmar huenda uharakishe utawala wa kiraia nchini humo. Kwa kuahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia katika kipindi cha miaka miwili, kamanda mkuu wa utawala wa Myanmar amezusha wasiwasi kuhusu hali ya baadaye ya utawala wa kijeshi ambao umekuwa ukiitawala nchi hiyo tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka wa 1962.
"Kwa kuwa katiba mpya tayari imeandaliwa, itapigiwa kura ya maoni mwezi ujao wa Mei na kufuatiwa na uchaguzi mkuu wa vyama vingi mwaka wa 2010 kwa mujibu wa katiba hiyo," amesema jenerali Than Shwe wakati alipowahutubia wanajeshi zaidi ya 13,000, wanadiplomasia na viongozi wengine mashuhuri waliokusanyika kwa ajili ya sherehe ya sikukuu ya majeshi ya Myanmar mnamo tarehe 27 mwezi uliopita.
Lakini jenerali Than Shwe alishindwa kutangaza tarehe ya kufanyika kura ya maoni wala kufichua lini wananchi watakaporuhusiwa kuiona katiba mpya ambayo imechukua muda wa miaka 14 kuitayarisha. Kuiokosoa katiba ni uvunjaji wa sheria na kosa linaloweza kusababisha kifungo cha hadi miaka 20 jela.
Sikukuu ya majeshi inayofanyika katika mji mkuu mpya wa Myanmar, Nay Pyi Daw, inaadhimisha kuundwa kwa jeshi la taifa mnamo mwaka wa 1945 chini ya shujaa wa uhuru jenerali Aung San Suu Kyi, baba aliyeuwawa wa kiongozi wa upinzani Bi Aung San Suu Kyi.
Kabla kuuhutubia umati wa watu, jenerali Than Shwe alikagua gwaride la heshima lililokuwa limesimama nyuma ya gari lake la kifahari aina ya limousine, lililoagizwa nchini Mynmar mahususi kwa sherehe ya sikukuu ya majeshi.
Hali mbaya ya afya
Hii huenda iwe siku ya mwisho ya majeshi kwa jenerali Than Shwe kama kamanda mkuu wa majeshi ya Myanmar kwa mujibu wa duru za kijeshi katika sherehe hiyo. Afya yake inaripotiwa kuzorota kwa kasi kubwa huku mara kwa mara akikabiliwa na matatizo ya kupumua na kusahau. Anaugua ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu. Figo zake zinashidhwa kufanya kazi ipasavyo na ana matatizo makubwa ya moyo.
Kulingana na wanadiplomasia waliohudhuria sherehe ya sikukuu ya majeshi ya Myanmar kuliwa na ushahidi kidogo wa matatizo yake ya kiafya wakati wa hotuba yake ya dakika 15 ingawa sauti yake ilisikika kuwa dhaifu kuliko kawaida. Hotuba ya jenerali Than Shwe imeelezwa kuwa fupi zaidi kuliko kawaida, jambo ambalo linaashiria matatizo ya kiafya yanayomkabili kamanda mkuu huyo.
Jenerali Than Shwe aliwataka wanajeshi waungane na wananchi kukandamiza kile alichokiita watu waharibifu wanaojaribu kuhujumu uthabiti wa taifa. Hakuyataja maandamano makubwa dhidi ya serikali yaliyoongozwa na watawa wa kibuda mnamo mwezi Septemba mwaka jana. Alimaliza hotuba yake kwa kusema jeshi la Myanmar lina kibarua cha kihistoria kutekeleza jukumu muhimu la kitaifa la kuibadili enzi na mfumo wa utawala kwa njia nzuri na hatua kwa hatua.
Mgogoro wazuka
Lakini chini ya ishara hii ya umoja ni mwanzo wa vita vipya kuhusu mustakabal wa Myanmar. Wakati huu vita hivyo sio kati ya watawa na jeshi kama ilivyokuwa mwaka jana, bali ni kati ya makundi mawili ndani ya jeshi la Myanmar. Katika miezi kadhaa iliyopita, mpasuko mkubwa umejitokeza ndani ya utawala wa kijeshi wa Myanmar kuhusu hali ya baadaye ya kisiasa ya taifa hilo.
Kitovu cha mgogoro huo ni wasiwasi kuhusu nani anayetakiwa kuusimamia mpango wa mabadiiliko ya kisiasa nchini Mynmar. Mivutano sasa imeanza kujitokeza kati ya viongozi wanaodhibiti utawala wa serikali ya Myanmar na matajiri wa nchi hiyo na wale wanaopendelea kujiona kuwa wasimamizi wa taifa hilo na wanaotaka kuilinda nchi kutokana na njama mbaya za maafisa wasioaminika.
Makundi mawili
Utawala wa kijeshi hauna umoja tena kama ilivyokuwa kwani kambi mbili zimeibuka. Upande mmoja kuna mawaziri na wanachama wa baraza la kitaifa la amani na maendeleo, SPDC, ambao wana masilahi makubwa ya kibiashara na wana mafungamano na muungano wa umoja na maendeleo, USDA, ulioasisiwa na jenerali Than Shwe.
Kwa upande mwingine kuna majenerali wa ngazi za juu wanaomuunga mkono naibu kamanda wa jeshi la Myanmar, jenerali Maung Aye, anayetaka jeshi liwe likifanya kazi ya kulipwa likiwa na jukumu kubwa la kuwalinda raia. Kundi hili limevunjwa moyo na ufisadi ndani ya serikali na linajua hali hii inafuja jukumu la baadaye la jeshi nchini humo.
Lakini kambi ya jenerali Muang Aye itatakiwa ichukue hatua za haraka ikiwa inataka kubakia kuwa na ushawishi mkubwa nchini. Kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mwezi ujao na uchaguzi mkuu katika miaka miwili utaubadili kabisa mtazamo wa kisiasa nchini Myanmar.
Muungano wa USDA, ambao hivi sasa unaandaa kura ya maoni na uchaguzi mkuu, utaongeza mamlaka yake na udhibiti wa mchakato mpya wa kisiasa unaojitokeza nchini Myanmar.