Mgogoro serikali ya Uingereza kuelekea Brexit
13 Juni 2017Wakati waziri mkuu Theresa May alipozindua kifungu cha 50 cha Mkataba wa Lisbon mwezi Machi, na hivyo kuanzisha mchakato rasmi wa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, hakujua kwamba muda si mrefu atakuwa anapigania maisha yake ya kisiasa.
Ibara ya 50 ambayo haikusanifiwa kurahisisha mambo kwa nchi yoyote inayotaka kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, inaweka muda maalumu wa miaka miwili wa mazungumzo, ikiipa Uingereza hadi Machi 2019 kukamilisha mazungumzo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameashiria kuwa hawataki kurefusha muda huo: "Hatujui lini mazungumzo ya Brexit yatakapaonza. Tunajua lini yanapaswa kumalizika," alisema rais wa baraza la Ulaya Donald Tusk kwenye ukurasa wa twitta siku ya Ijumaa.
Hatari ya mchakato kuvurugika zaidi
Mazungumzo yalitarajiwa kuanza Juni 19, lakini matokeo ya kushitukiza ya uchaguzi Juni 9 ambamo Wahafidhina walipoteza wingi wao bungeni, hilo linazidi kutowezekana. "Hakuna shaka kabisaa kwamba Uingereza inaingia katika majadiliano hayo ikiwa dhaifu, na kukosekana kwa mamlaka ya wazi kunahatarisha kuvuruga zaidi mchakato ambao tayari ulionekana kuwa mgumu," amesema Sophie Gaston, mkuu wa miradi ya kimataifa kutosha shirika la ushauri la Demos.
Amesema hatua ya May kuzindua ibara ya 50 kabla ya uchaguzi ilikuwa ya kiburi na imeiacha nchi hiyo ikiwa katika nafasi dhaifu kabisaa. Amesema inawezekana wakachelewesha kuanza kwa majadiliano kadiri wapendavyo, lakini muda hautasimama kwenye tarehe yake ya mwisho.
May anataka kubuni muungano na chama cha Democratic Union cha Ireland ya Kaskazini DUP, ambacho kitawaimarisha Wahafadhina katika serikali ya wingi mdogo, lakini ambayo bado haina uhakika. Wakati majadiliano na DUP yakiendelea, May amekamilisha muundo wa baraza lake la mawaziri.
Njia ya mashaka
Bado haijajulikana ni athari zipi nafasi hii iliopungua ya chama cha Conservative itakuwa nazo kuhusu mazungumzo ya Brexit. Baadhi ya wadadisi wameyafasri matokeo ya uchaguzi kama kukataliwa kwa mkakati wa May mpaka sasa - lakini ni taswira mchanaganyiko.
Licha ya ukubwa wa changamoto ya kikatiba inayoikabili Uingereza, ushirikiano kati ya vyama hauonekani kuwa kwenye agenda, mnamo wakati uahasama wa kivyama unazidi kuongezeka. Gaston anasema lingekuwa jambo la manufaa kwa taifa kuwa na vichwa bora vikishirikiana - lakini mashaka na fursa yanavyotoa matokeo hayo ya vurugu kwa Conservatives na Labour vinamaanisha kuwa kutakuwa na ari kubwa ya kivyama kutoka pande zote mbili.
Wakati May akipambana kubakia madarakani, maswali yameanza kuulizwa kuhusu uwezo wake wa kuongoza Uingereza kupita katika kipindi hiki. Mwanasheria ambaye pia ni mtangazi David Allen Green, aliiambia DW kuwa hasara itakayosabishwa na Brexit itasababishwa zaidi moja kwa moja na mfululizo wa maamuzi mabaya ya May kuliko matokeo halisi ya kura ya maoni.
Anasema wakati Uingereza ikiwa katika mwezi wa tatu wa mchakato wa Ibara ya 50, inaonekana taifa hilo liko katika nafasi mbaya zaidi kutokana masihara ya May ya uchaguzi mkuu kuliko wakati Uingereza ilipotoa taarifa hiyo.
Mwandishi: Samira Shackle, DW
Ripoti: Iddi Ssessanga
Mhariri:Caro Robi