Saudia yamtaka balozi wa Canada kuondoka nchini mwake
6 Agosti 2018Wizara ya mambo ya kigeni ya Saudi Arabia imesema itafungia biashara zote mpya kati ya nchi yake na Canada. Asilimia 10 ya mafuta ghafi yanayoingizwa Canada yanatokea Saudi Arabia.
Kwa wakati huu haijawa wazi ni biashara gani mpya zitakazoathiriwa na mgogoro huu kati ya nchi hizi mbili, lakini uhusiano wao wa pamoja wa biashara, ulifikia dola bilioni 3 mwaka 2016 huku matanki ya kijeshi na magari ya kivita yakiwa miongoni mwa bidhaa zinaingizwa Saudi Arabia kutoka Canada hii ikiwa ni kulingana na takwimu za serikali.
"Hatua yoyote itakayochukuliwa na Canada kuelekea mwelekeo huo, tutaichukulia kama haki yetu na sisi kuingilia masuala ya ndani ya Canada'', ilisema wizara ya mambo ya kigeni ya Saudi Arabia, na kuongeza kuwa Canada na nchi nyengine zote zinahitaji kujua kwamba haziwezi kujifanya zinawajali zaidi watu wa taifa hilo kuliko nchi hio inavyowajali watu wake.
Haijajulikana iwapo balozi wa Canada Dennis Horak yupo bado Saudi Arabia, lakini taifa hilo limesema pia litamrejesha nchini balozi wake aliyeko Canada.
Hata hivyo Marie-Pier Baril, msemaji wa waziri wa mambo ya nje wa Canada Chrystia Freeland, amesema nchi yake ina wasiwasi juu ya hatua zinazochukuliwa na Saudi Arabia.
Amesema bado taifa lake litaendelea kutetea haki za binaadamu ikiwemo haki za wanawake pamoja na uhuru wa kujieleza duniani kote. Msemaji huyo ameongeza kuwa serikali yake haitasita kulinda maadili ambayo ni muhimu kwa diplomasia ya Kimataifa.
Bahrain yasema ipo pamoja na Saudi Arabia dhidi ya wanaotaka kuukandamiza uhuru wa taifa hilo.
Mgogoro huo kati ya Saudi Arabia na Canada unaonekana kuchochewa na maneno katika mtando wa twitter wa baadhi ya wajumbe wa Canada wakitaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo kwa wanaharakati wa kike wa kutetea haki za binaadamu waliozuiliwa hivi Karibuni nchini Saudi Arabia.
Miongoni mwa wale waliotiwa nguvuni ni pamoja na Samar Badawi, ambaye kakaake Raif Badawi alitiwa nguvuni Saudi Arabia mwaka 2012 na baadaye kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela pamoja na viboko 1000 kwa kosa la kuwakosoa viongozi wa kidini. Mkewe Ensaf Haidar, kwa sasa amehamia nchini Canada.
Wakati huo huo Bahrain imesema inasimama pamoja na Saudi Arabia katika mgogoro wake wa kisiasa na Canada. Wizara ya kigeni ya nchi hiyo jirani wa Saudi Arabia katika Ghuba ya Uarabu, imethibitisha hilo kupitia mtandao wake wa kijamii wa twitter ulioandikwa kuwa Bahrain ipo pamoja na taifa hilo la kifalme dhidi ya mtu yeyote anayejaribu kukandamiza uhuru wake.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel