1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Syria Magazetini

6 Februari 2012

Kura ya turufu ya Russia na China dhidi ya mswaada wa nchi za magharibi na za kiarabu dhidi ya Syria na athari za kukeketwa wasichana ndizo mada zilizohanikiza magazetini hii leo nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/13xlF
Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuhusu SyriaPicha: dapd

Hakuna hata gazeti moja la humu nchini ambalo halijachambua kwa kina sababu zilizopelekea Russia na China kutumia kura zao za turufu kuzuwia azimio la nchi za magharibi na za kiarabu dhidi ya Syria lisipite katika baraza la usalama.Tuanzie na gazeti la "Landeszeitung" la mjini Lüneburg linalohisi:"Kura mbili za turufu  zimesababisha kiwingu cha kiza kutanda juu ya jumuia ya kimataifa na kuzusha kwa mara nyengine tena suala kama haki ya kumiliki kura ya turufu ambayo madola makuu yamekuwa yakijivunia tangu vita vikuu vya pili vilipomalizika, inaweza kubatilishwa. Damu imeganda mikononi mwa madola mawili yenye kumiliki kura ya turufu- Russia na China- damu ya wapinzani wa Syria waliouliwa kwa maelefu na muimla Bashar Assad. Sababu za kiuchumi na kisiasa ndizo zilizowafanya viongozi wa Moscow na Beijing waseme "la".Kwa warusi, ni kwa sababu ya kampeni za uchaguzi zinazoendelea na wasi wasi wa kuzidi kupoteza ushawishi ulimwenguni. Lakini bila shaka si kwasababu ya misingi ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyengine. Kama ndio hivyo, basi waliiweka wapi sheria ya kimataifa walipoingia kijeshi nchini Georgia mnamo mwaka 2008?

Syrien Proteste Demonstrationen Russland Putin Bashar Assad
Waandamanaji wamebeba bango la picha ya waziri mkuu wa Urusi,Vladimir Putin akimsaidia Bashar al AssadPicha: AP

Gazeti la "SÜDWEST PRESSE" la mjini Ulm linazitaja pia sababu za kiuchumi kuwa ndio sababu ya msimamo wa Russia na China. Gazeti linaendelea kuandika:"Shinikizo la kimataifa  dhidi ya mtawala wa Damascus limepwaya tangu mwishoni mwa wiki. Biashara ya silaha za Russia inaweza kwa hivyo kuendelea bila ya pingamizi, China inayaangalia kijicho pembe mafuta ya Syria, wachunguzi waliokuwa wakiudhi wa nchi za kiarabu wameshakwenda zao na waandishi habari wachache tu ndio wanaoingia nchini humo. Badala yake utawala wa Assad umepata nafasi sasa ya kuendelea kuwaandama wapinzani wake bila ya tahayuri wala mashahidi. Mauwaji ya Homs ni mwanzo tu. Rais Bashar al Assad hataoweza tena kuirejesha Syria katika maisha yaliyostawi ya jamii.Yeye na kundi lake la watawala wanaowauwa maelfu ya raia, kuwatesa na kuwatokomeza korokoroni, hawana tena hatima njema, licha ya kupata msaada wa silaha na wa kidiplomasia kutoka Moscow na Beijing

Sensibilisierung im Dorf mit einem Theaterstück FGM
Kampeni dhidi ya kukeketwa wasichana Guinea BissauPicha: DW

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mila za kukeketwa wasichana. Gazeti la "Fränkischer Tag" la mjini Bamberg linaandika:Takriban asili mia 80 ya wasichana wanaoishi Ujerumani na ambao wana asili ya  Somalia,Ethiopia au Sierra Leone wanahofia wakenda likizo katika nchi wazee wao walikotokea, na wao pia wanaweza kukumbwa na balaa la kukeketwa. Wasichana, watoto wa jirani, watoto wanaokwenda darasa moja na watoto wetu. Kukeketwa wanawake si chochote chengine isipokuwa kumtesa mtu makusudi-kitendo ambacho hakistahiki kamwe kuvumiliwa-ni uhalifu unaobidi kuandamwa mahakamani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri. Miraji Othman