Mgogoro wa wakimbizi wavigawa vyama vya kihafidhina Ulaya
23 Oktoba 2015Kama ilivyo kawaida, mkutano mkuu wa muungano wa vyama vya kihafidhina vya Ulaya EEP, uliyofanyika mjini Madrid jana, ulipangwa kuwa sherehe ya kifamilia, na pia kama mkakati wa kumuimarisha waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy, ambaye anawania kuchaguliwa tena Desemba 20. Lakini mgogoro unaoendelea wa wakimbizi uliubadili haraka mkutano huo na kuwa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi wa kihafidhina -- waliokuwepo kwa wingi, kuhusu wakimbizi.
Kabla ya kuwasilisha misimamo yao kwa wajumbe wa EEP, kundi dogo la viongozi walikutana kwa siri. Washiriki wanasema mkutano huo wa siri uligubikwa na ushari. Baadaye jukwani kwenye ukumbi mkubwa, maelewano yalitawala. Mabango makubwa ya rangi ya blu yenye maneno yasemayo "pamoja", yalionyesha ni namna gani wahafidhina, wanaotawala katika karibu nusu ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya walikuwa wakitafuta.
Merkel: Kila moja laazima atendewe kama mwanadamu
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisisitiza msimamo wake kwamba mipaka laazima iendelee kuwa wazi, na kwamba hakuwezi kuwepo na kiwango cha mwisho cha idadi ya wakimbizi na watafuta hifadhi wanaoweza kuchukiwa na Umoja Ulaya.
"Kila anaewasili Ulaya ana haki ya kutendewa kama mwanadamu. Hatukuunda mkataba wa haki za msingi ili tuwatendee watu kutoka sehemu nyingine za dunia kama wanyama," Merkel aliwambia wawakilishi wa vyama 75 kutoka mataifa 40.
Alirejea moto yake ya "Tunaliweza hili!" na kusema pia kwamba Umoja wa Ulaya utapaswa kushirkiana na Uturuki na kuurejesha mpaka kati ya washirika wa NATO Uturuki na Ugiriki katika hali ya kisheria. Maelfu ya wakimbizi huwasili katika visiwa vya Ugiriki kwa boti kila siku.
Merkel hakuitaja hali ya machafuko katika njia ya Balkan. Lakini alitoa wito wa jumla kwa wenzake kuwa na umoja na kukubali kuugawana mzigo wa wakimbizi kwa usawa, ambapo kila mmoja atatoa mchango kulingana na uwezo wake.
"Imekuwa hivyo barani Ulaya na hii ndiyo njia ya mafanukio," alisema Merkel na kuongeza kuwa hatoacha kupambana, kuhakikisha wanaumudu mgogoro huo, ambao pengine unawakilisha changamoto yao kubwa zaidi katika miongo kadhaa.
Orban: Ulaya ni dhaifu
Waziri mkuu wa Hungary hakumumunya maneno yake kuhusu ukweli kwamba anadhani hii ni sera isiyo sahihi, na kutoa wito wa kuimarisha ulinzi kwenye mipaka ya nje ya Umoja wa Ulaya kuzuwia mmiminiko wa wakimbizi. Alisema ikiwa hili haliwezi kufanyika nchini Ugiriki, basi Hungary na Slovenia zitalifanya zenyewe. "Ulaya ni tajiri na dhaifu, na huu ndiyo mchanganyiko hatari zaidi," alisema Orban.
Alisema wanachokabiliana nacho sasa siyo mgogoro wa wakimbizi, bali ni vuguvugu la uhamiaji linalojumlisha wahamiaji wa kiuchumi, wakimbizi na hata wapiganaji wa kigeni. Alisema ingawa heshima ya hadhi ya mtu na usalma ni haki za msingi, si mfumo wa maisha wa Ujerumani wala Hungary ni haki ya msingi kwa watu wote duniani.
"Ni vuguvugu la wahamiaji na siyo wakimbizi"
Alisema hana chuki yoyote na Waislamu, lakini aliongeza kuwa "hatuna mamlaka ya kuibadili jamii ya Ulaya." Akimjibu Kansela Merkel, waziri mkuu huyo wa Hungary alisema mtu hawezi kutoa ahadi asizoweza kuzitekeleza. Aliendelea kusema kuwa wengine wa wahamiaji hao hawaonekani kama wakimbizi kutoka Syria, lakini "wanaume vijana wanaoonekana kama jeshi."
Mwenyekiti wa kundi la EEP katika bunge la Ulaya Manfred Weber kutoka chama cha CSU cha Ujerumani, alikiri kuwepo na mvutano ndani ya familia ya chama chake. "Hali ndani ya EEP haina utofauti na kwingineko barani Ulaya. Tuko katika uhusiano wa mvutano mkali sasa hivi," Wever aliiambia DW katika mahojiano.
Karibu watu 600,000 wanakimbia vita na umaskini, wengi wao wakiwa wakimbizi kutoka vita vya Syria, wamewasili barani Ulaya mwaka huu, ambapo idadi kubwa kati yao wakielekea Ujerumani na Sweden.
Hungary imeitikia wimbi hili kubwa zaidi la wakimbizi barani Ulaya tangu kumalizikiwa kwa vita kuu vya pili vya dunia, kwa kujenga uzio wa chuma kwenye mipaka yake na Serbia na Croatia, hatua iliyokaribishwa na pia kukosolewa na viongozi mbalimbali barani Ulaya.
Mwandishi: Bernd Riegert/Iddi Ssessanga/AFP,EAPE
Mhariri: Saumu Yusuf