Mgombea wa upinzani Uganda alalamikia unyanyasaji wa polisi
2 Desemba 2020Mgombea huyo maarufu kama Bobi Wine alisitisha kampeni zake hapo jana wakati walinzi wake wawili walipojeruhiwa na kile kinachodaiwa kuwa vilipuzi walivyotupiwa na polisi. Hata hivyo polisi imekanusha madai hayo ikisema kuwa kuna baadhi ya raia walio na vilipuzi kama hivyo.
Hali ilikuwa ya taharuki tangu asubuhi kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi pamoja na yale ya chama cha NUP wafuasi wa chama hicho wakisubiri matokeo ya mashauriano kati ya viongozi wao na wakuu wa tume ya uchaguzi. Viongozi wa NUP wakiongozwa na Bobi Wine waliwasilisha ushahidi kuhusu mienendo ya vyombo vya usalama kwa kuwahangaisha kila wanakokwenda kuendesha kampeni zao kwa mujibu wa ratiba na sheria walizopewa na tume hiyo. Waandishi wa habari hawakuruhusiwa katika kikao hicho lakini ulipokamilika.
Mgombea Bobi Wine asitisha kampeni zake nchini Uganda
Hapo jana Bobi Wine alisitisha kampeni zake baada ya walinzi wake wawili na wafuasi kadhaa kujeruhiwa mjini Jinja. Ameitaka tume ya uchaguzi ihakikishe kuwa vyombo vya usalama vinaheshimu haki yake kutafuta kura. Huku baadhi ya wafuasi wa chama chake wakipendekeza uchaguzi uahirishwe kwani mazingira ya sasa si salama kwa zoezi huru na la amani la kidemokrasia.
Kwa upande wao polisi wanasisitiza kuwa wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa katika kuendesha kampeni na hawaonekani kukubali lawama zozote wanazotupiwa. Huku kampeni hizo za urais zikingia wiki ya nne, angalau wagombea wote dhidi ya rais Museveni wamejikuta wakikabiliana na vyombo vya usalama pale wanapozuiliwa kuwafikia wananchi kuwaelezea sera zao lakini Bobi Wine ndiye ambaye ameonekana kuandamwa zaidi anasema.
Soma zaidi:Museveni na Bobi Wine walaumiana kuhusu vifo vya raia
Kwa upande wake, rais Museveni ameendesha kampeni zake akikutana tu na viongozi wa wilaya na kanda.
Chanzo: DW