Mgomo wachafua sherehe za krismasi Ufaransa
26 Desemba 2019Watu wengi wamehangaika katika dakika ya mwisho kutafuta njia mbadala wakati maandamano dhidi ya mageuzi ya pensheni yakishuhudia maelfu ya treni zikifutwa ama kucheleweshwa , na taksi, huduma za kusafiri na wenye magari na mashirika ya magari ya kukodi yakishindwa kujaza pengo la upungufu wa matreni.
ni sehemu ndogo tu ya treni za mwendo kasi na treni zinazosafiri kati ya miji mikuu zilitembea katika mkesha wa sikukuu ya Krismasi na hata treni chache zaidi zilifanyakazi katika sikukuu yenyewe jana. Vituo vikuu vya treni mjini Paris vilifungwa majira ya asubuhi ambapo huduma za kwenda maeneo ya mashambani zilipunguzwa na ni njia mbili tu kati ya 16 za treni , zile ambazo hazina dereva ndio zilikuwa zinafanyakazi.
rais Emmanuel Macron alitoa wito wa suluhu wakati huu wa sikukuu , lakini majadiliano kati ya serikali na vyama vya wafanyakazi wiki iliyopita yalishindwa kupata msimamo wa pamoja.
Wagomaji waapa
Na wagomaji waliapa kwamba hakutakuwa na kusimamisha mgomo wakati wa kipindi hiki cha sikukuu hadi pale maafisa watakapoondoa mipango ya kuunganisha mifumo 42 ya pensheni kuwa mmoja.
Usafiri siku ya Alhamis utaendelea kuwa wa shida, ambapo ni treni moja kati ya mbili zendazo kasi zitafanyakazi, njia tano za treni mjini paris zitafungwa na huduma za treni za mikoani na mijini pia zitaathirika.
Mazungumzo yanapangwa kuanza tena hapo Januari 7.
Serikali inasema mabadiliko ni lazima ili kujenga mfumo wenye usawa wa pensheni.
Lakini wafanyakazi wengi wanapinga kujumuishwa kwa kile kinachoitwa umri wa mwisho wa kustaafu wa miaka 64 ambapo watu wanalazimika kufanyakazi ili kuweza kupata malipo kamili ya pensheni, miaka miwili kupindukia umri rasmi wa kustaafu.