1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 10 tangu Gaddafi kuuawa, Libya ingali inayumba

Angela Mdungu Kersten Knipp
20 Oktoba 2021

Kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar al-Gaddafi aliuwawa miaka 10 iliyopita. Tangu wakati huo, taifa hilo halijawahi kuachana na mzozo unaolikabili.

https://p.dw.com/p/41ucF
Muammar al-Gaddafi
Picha: Getty Images/AFP/C. Simon

Hata uchaguzi wa bunge na Rais uliokuwa umepangwa ufanyike mwezi Desemba umeahirishwa. Zaidi kuhusu mgogoro huo ni uchambuzi wa mwandishi wa DW Kersten Knipp.

Kifo cha mtawala wa Libya, Muammar al Gaddafi, kilitangazwa miaka kumi iliyopita, Oktoba 20, 2011. Miezi michache kabla ya kifo chake, watu wa Libya waliokuwa na shauku ya mabadiliko walianzisha vuguvugu wakivutiwa na kilichotokea katika nchi jirani ya Tunisia, wakipinga utawala wa kiongozi huyo aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1969 ambapo aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi.

Waasi dhidi ya serikali yake, walikuwa na washirika wenye nguvu: mnamo mwezi Machi, Umoja wa mataifa ulitoa ruksa wa kufanyika kwa oparesheni ya kijeshi.  Operesheni hii ilidhamiria kuwalinda raia. Kisha mashambulizi dhidi ya jeshi la Gaddafi yaliendeshwa  na Jumuiya ya kujihami ya NATO hali iliyodhoofisha utawala wake kwa kiasi kikubwa.

Baada ya miezi mingi ya kukimbia, Gaddafi hatimaye alijificha katika mji wa Sirte kaskazini mwa Libya, kilometa 450 mashariki mwa mji mkuu Tripoli. Akiwa amezungukwa na mahasimu wake, alijaribu kutoroka kupitia mfereji wa maji taka lakini alikamatwa. Waasi walimuuwa haraka na kinyama huku picha yake iliyotapakaa damu ikisambaa kote ulimwenguni.

Kutokuridhishwa sehemu kubwa ya watu wa Libya katika utawala wa Gaddafi kulitokana na sababu za kiuchumi na kijamii kama vile kupanda kwa bei za vyakula na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kama anavyosema mtafiti na mtaalamu wa masuala ya Libya wa taasisi ya masuala ya Mashariki ya kati ya mjini hamburg Hager Ali.

Shauku ya matumaini ya mwanzo mpya katika siku za awali ilikuwa kubwa, lakini kulitolewa kauli za tahadhari kama alivyowahi kunukuliwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo Ban Ki Moon

Kifo cha mtawala wa Libya, Muammar al Gaddafi, kilitangazwa miaka kumi iliyopita, Oktoba 20, 2011.
Kifo cha mtawala wa Libya, Muammar al Gaddafi, kilitangazwa miaka kumi iliyopita, Oktoba 20, 2011.Picha: ADEM ALTAN/AFP/Getty Images

"Safari iliyoko mbele ya Libya na watu wake itakuwa  ngumu na yenye changamoto nyingi. Watu wa Libya watapaswa kufanyakazi pamoja. Walibya wanaweza kufikia malengo ya mustakabali wao kupitia umoja wa kitaifa na upatanishi. Pande zote zinazopingana zinapaswa kuweka chini silaha. Huu ni wakati wa kuponya majeraha na kujenga upya kwa ukarimu na si kwa kisasi," alisema Moon

Licha ya tahadhari hiyo mnamo mwaka 2014, mzozo nchini humo uligeuka kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoendelea kwa miaka mingi.

Matokeo yake, Libya imekwama kama taifa. Serikali ilisambaratika. Muda mfupi baadaye kukawa na serikali mbili. Moja katika mji mkuu Tripoli, na nyingine katika mji wa pwani wa Tobruk mashariki mwa nchi hiyo. Ili kulinda ama kutekeleza maslahi yao, mataifa ya kigeni yakaanza kuingilia vita. Baadhi ya wanajeshi wao wakiwemo mamluki bado wamo nchini humo.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa mfano alijaribu kuvichukua visima vya mafuta katika bahari ya Mediterranean kupitia ushirika wake na mmoja wa viongozi wa serikali hiyo mbili za Libya, Fajis al-Sarradsch. Serikali ya Misri kwa upande wake iliunga mkono serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayohusishwa na kamanda mbabe wa vita, Khalifa Haftar. Kwa kufanya hivyo Misri ilikuwa na matumaini ya kuvimudu vikosi vya kiislamu hasa kundi la Udugu wa kiislamu.

Ulaya kwa upande wake kimsingi inataka kuhakikisha kuwa Libya haiwi kituo kipya cha wakimbizi kuingia barani humo kisicho na udhibiti kama alivyosema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Haiko Maas Februari 2020

Mwandishi: Kersten Knipp

Tafsiri: Angela Mdungu

Mhariri: Mohammed Khelef