Michezo: Bundesliga na Ligi za Ulaya
5 Novemba 2010Viongozi wa ligi ya Ujerumani Borussia Dortmund wana pania kuendeleza kuiongoza ligi wiki ijaayo katika mpambano wao na Hanover siku ya Jumapili. Chipukizi Mainz ambayo wanawahemea Dortmund mgongoni, wana hamu ya kuendelea kuwa kileleni baada ya kichapo wiki iliopita mikononi mwa Dortmund wanakutana na Freiburg Jumamosi hii. Katika mechi zingine mabingwa watetezi Bayern Munich ambao wanatamba Ulaya lakini wamekuwa wakisuasua katika Bundesliga wana miadi leo na Borussia Moenchegdlabach inayoburura mkia. Hamburg wanawaalika Hoffenhiem, ilhali Cologne imesafiri hadi Nuremberg. Kesho VFB Stuttgart wako nyumbani na Werder Bremen. Ilhali Bayer Leverkusen watawaalika Kaisersslautern.
Huko Uingereza Mabingwa Chelsea watakuwa uwanjani Anfield dhidi ya Liverpool siku ya Jumapili ambao wanaonekana wameanza kuamka toka usingizini hasa baada ya kushinda mechi zao mbili na kuondosha wasiwasi wa kushushwa daraja.
Katika mechi za Jumamosi, Bolton watamenyana na Tottenham ambao wana moto hasa baada ya ushindi wao dhidi ya mabingwa wa Ulaya Inter Milan katika Champions League kati kati ya wiki. Birmingham itacheza na West Ham, Wigan itawaalika Blackburn ilhali Manchester United watakuwa nyumbani dhidi ya Wolves. Jumapili Arsenal pia watakuwa nyumbani dhidi ya Newcastle.
Nchini Spain mchezaji wa kimataifa Ruben de la Red amestaafu kusakata kabumbu kutokana na matatizo ya moyo. De la Red ambaye alikuwa anaichezea Real Madrid alianguka na kupoteza fahamu wakati timu hiyo ilipokuwa inacheza mechi ya kombe la Kings Oktoba 2008.
Madrid imesema de la Red atasalia Bernabue na kujiunga na timu ya makocha inayosimamiwa na Jose Mourinho. Spain ina historia ya kuwa na wachezaji wenye matatizo ya moyo. Katika miaka miwli iliopita wachezaji wawili wamekufa kutokana na matatizo ya moyo walipokuwa uwanjani.
Barani Afrika- Shirikisho la kandanda nchini Nigeria NFF limemteua Samson Siasia kama kocha mpya wa timu ya taifa. Mbali na Siasia, mchezaji wa zamani wa Super Eagles Stephen Keshi pia alikuwa mbioni kuwa kocha wa timu ya Nigeria. Siasia amekuwa kocha wa timu ya Nigeria ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 na pia alikuwa kocha wa timu iliyoiwakilisha Nigeria katika michezo ya Olimpiki 2005 na 2009.
Kibarua cha kwnaza cha Siasia ambaye ametia saini kandarasi ya miaka minne itakuwa kuhakikisha Nigeria inafuzu kwa kombe la mabingwa barani Afrika litakaloandaliwa nchini Libya 2012.
Nigeria ipo katika nafasi ya pili katika kudni B nyuma ya Guinea. Kundi hilo pia linazijumuisha Madagascar na Ethiopia.
Mchezaji wa kiungo cha kati na nahodha wa Black Stars Michael Essien bado hajaamua kurejea katika timu ya taifa na atakosa mechi ya kirafiki kati ya Ghana na Saudi Arabia.
Essien anayesakata dimba lake Chelsea aliwaambia maafisa wa kandanda wa Ghana kwamba bado anahitaji mapumziko kurejea kuichezea timu hiyo ya taifa. Essien alikosa kombe la dunia nchini Afrika Kusini kwa kuwa alikuwa anaguza jeraha la goti.
Essien hajaichezea Ghana katika mechi tatu walizocheza tangu waondoke Afrika Kusini baada ya kuondolewa katika robo fainali ya Kombe la dunia. Ghana imetangaza timu ya wachezaji 19 itakayokutana na Saudia Arabia huko Dubai novemba 17.
Na Essien hayuko pekee yake, mwenzake wa Chelsea Didier Drogba wa Ivyory Coast pia amesema anahitaji mapumziko kutoka timu ya taifa. Drogba hajaichezea tembo ya Ivory Coast tangu kumalizika kwa kombe la dunia. Ivory Coast ina mechi ya kirafiki dhidi ya Poland pia tarehe 17 mwezi.
Mwandishi: Munira Muhamamd/RTRE
Mhariri: Josephat Charo.