Michuano ya kombe la Afrika kuanza Libreville
14 Januari 2017Wenyeji wa mashindano Gabon wanapaswa kujiweka imara kiakili wakati watakapopambana na wapinzani hao ambao hawafahamiki sana katika soka la Afrika Guinea Bissau wakati wanawania kuanza vizuri kampeni yao wakati fainali za kombe hilo zitakapofunguliwa rasmi kwa michezo miwili leo Jumamosi(14.01.2017).
"Kuna mbinyo mkubwa lakini ni vizuri kwamba tunacheza nyumbani. Tuna mkandamizo mkubwa wa mawazo na majukumu," mlinzi wa Gabon Bruno Ecuele Manga alisema katika mkesha wa mchezo wao leo.
Kombe la mataifa ya Afrika linaelekea kuzowea kufanyika nchini Gabon , likirejea katika taifa hilo ambalo lilikuwa koloni la zamani la Ufaransa katika pwani ya magharibi ya Afrika kwa mara ya pili katika mashindano manne yaliyopita. Gabon ilifanya kazi nzuri kuwa wenyeji wenza pamoja na Guinea ya Ikweta mwaka 2012 na mwaka huu inafanya kazi hiyo peke yake baada ya Libya inayokumbwa na vita kuamua kujitoa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Wapinzani hao wa Gabon Guinea Bissau wanawania kuendeleza mafanikio yao waliyoyapata katika michezo ya mchujo. Guinea Bissau ni moja kati ya nchi masikini sana barani Afrika na matayarisho yao wamekumbwa na matatizo ya fedha, ikiwa ni pamoja na mgomo wa wachezaji wiki iliyopita.
Matumaini ya robo fainali
Burkina Faso na Cameroon zinapambana katika mchezo wa pili wa kundi A katika uwanja unaoweza kuingiza mashabiki 40,000 wa Stade de I'Amitie, mjini Libreville, timu zote zikiwa na matumaini ya kushinda na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga katika nusu fainali.
"Iwapo tutashinda mchezo huu tayari tutakuwa na asilimia 50 ya kuingia katika robo fainali," amesema kocha wa Cameroon Hugo Broos. Michezo ya leo Jumamosi inazindua wiki tatu za heka heka za mapambano ya kuwania kombe la mataifa ya Afrika kuamua nani atakuwa bingwa mpya wa bara la Afrika katika fainali itakayofanyika mjini Libreville hapo Februari 5.
Ghana imewahi kukaribia kupata mafanikio baada ya kuonesha mchezo mzuri katika fainali tano za kombe hilo la Afrika lakini imeshindwa kulinyakua kila mara, hali inayotoa changamoto kubwa na pia motisha kwa kikosi hicho cha Black Stars wakati wakiwania tena kulinyakua kombe hilo mara hii.
Tembo wa Cote d'Ivoire
Kikosi kipya cha Tembo wa Cote d'Ivoire kinajitayarisha kutetea ubingwa wao wa kombe la Afrika , wakichochewa na matokeo mazuri na kiwango cha juu cha timu yao kutoka kwa mchezaji mpya Wilfried Zaha.
Mshambuliaji huyo wa timu ya Crystal Palace anamatumaini ya kuweka alama yake katika mashindano hayo ambayo yanajumuisha wachezaji kadhaa wanaocheza soka katika mataifa ya Ulaya kama Riyad Mahhrez wa Algeria , Pierre -Emerick Aubameyang wa Gabon na Sadio Mane wa Senegal.
Zaha ni mchezaji muhimu aliyeongezwa katika kikosi hicho kwa kuwa nyota wengi wa zamani kama ndugu wawili Toure , Kolo na yaya wamejiuzulu na mshambuliaji nyota wa pembeni Gervinho ni majeruhi.
Zaha aliyezaliwa mjini Abidjan ameshawishiwa kushiriki katika kombe la mataifa ya Afrika na uwezekano wa mafanikio katika kombe hilo na kombe la dunia baada ya kushiriki katika michezo miwili ya kirafiki katika timu ya nchi anakoishi hivi sasa England.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Zainab Aziz