1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

070610 Vorschau WM Südafrika

Josephat Nyiro Charo11 Juni 2010

Nchini Afrika kusini hii leo Ijumaa tarehe 11.06.10 yanafunguliwa rasmi kwa mara ya kwanza katika ardhi ya bara la Afrika mashindano ya fainali za kombe la dunia la kandanda.

https://p.dw.com/p/No6h
Rais wa FIFA, Sepp Blatter, kulia, na rais wa Afrika Kusini, Jacob ZumaPicha: AP

Firimbi ya kuanzisha mashindano hayo itakapolia jioni hii wenyeji wa mashindano hayo Afrika Kusini watapambana na Mexico katika mchezo wa kwanza. Hali hii ya kufurahia mashindano haya makubwa ilikuwa na shaka wakati wote wa maandalizi, iwapo Afrika Kusini ilikuwa tayari kwa ajili ya changamoto ya mashindano makubwa kama haya.

Afrika kusini ilianza rasmi sherehe hizi za kombe la dunia jana Alhamis kwa shamrashamra za burudani ya muziki iliyosheheni wanamuziki nyota kutoka sehemu mbali mbali duniani, ikiwa ni pamoja na Shakira, na kundi linaloungurumisha muziki wa Afropop kutoka nchini Afrika Kusini wakifunga tamasha hilo kwa wimbo rasmi wa fainali hizo, Waka Waka.

Kitongoji cha Soweto, eneo ambalo litafanyika mchezo wa ufungizi wa fainali hizi, lilikuwa katika hali ya sherehe kubwa jana kwa tamasha la muziki. Shakira mzaliwa wa Colombia, mwimbaji wa muziki wa rap K'naan mzaliwa wa Somalia na mwimbaji wa muziki wa soul, Alicia Keys, walitia fora. Afrika Kusini inafurahia muziki, Afrika kusini ni poa, amesema hayo rais wa Afrika kusini Jacob Zuma alipowahutubia mashabiki 34,000 waliohudhuria burudani hiyo katika mkesha wa ufunguzi wa mashindano ya fainali za kombe la dunia.

Waziri wa utalii wa Afrika kusini Marthinus van Schalkwyk alikuwa na haya ya kusema, "Zitakuwa fainali adimu za kombe la dunia la FIFA mwezi huu wa Juni na Julai. Lakini pia itakuwa juu ya kupata uzoefu wa kipekee kuhusu Afrika."

Bafana Bafana timu ya taifa ya Afrika Kusini inapambana na Mexico katika pambano la ufunguzi katika uwanja wa Soccer City katika kitongoji cha Soweto wakati Ufaransa ikiwa na miadi na Uruguay baada ya pambano hilo la ufunguzi.

Flash-Galerie WM Fans
Washabaki wa Bafana Bafana, timu ya Afrika KusiniPicha: AP

Rais Jacob Zuma ana matumaini ya kumkabidhi kombe nahodha wa Afrika Kusini Aaron Mokoena hapo Julai 11, lakini wengi wa mashabiki wa Afrika Kusini wanaamini kuvuka duru ya kwanza litakuwa jambo jema kabisa.

Didier Drogba amerejea katika mazoezi kiasi siku chache baada ya kufanyiwa upasuaji katika mkono wake uliovunjika na huenda akafikiriwa kushiriki katika mchezo wa kwanza wa Ivory Coast dhidi ya Ureno.

Mabingwa wa Ulaya Hispania wameondoka jana Alhamis kuelekea nchini Afrika Kusini wakiwa hawataki kujitutumua kuwa wanapigiwa upatu kushinda kombe hilo la dunia.

Ujerumani ikiwa ni moja ya timu zinazofikiriwa kuwa huenda zikanyakua kombe hilo pamoja na Hispania na Brazil iko tayari kwa fainali hizo anasema kocha wa timu hiyo Joachim Löw.

Sisi kama Wajerumani tumo miongoni mwa wale wanaopigiwa upatu kulinyakua kombe hili, bila shaka. Na tunataka kulinyakua.

Masuala ya kifamilia pia yanahusika katika fainali hizi za kombe la dunia 2010 wakati Slovakia na Marekani zina makocha ambao katika timu zao kuna watoto wao. Mataifa matatu yana ndugu wanaocheza katika timu hizo na ndugu wawili watapambana katika timu tofauti. Kocha Vladimir Weiss katika kikosi chake yumo mwanawe anayekwenda kwa jina la Vladimir Weiss pia ambaye huchezea klabu ya Manchester City.

Kikosi cha Marekani, US Boys kikiongozwa na kocha Bob Bradley kinamjumuisha pia mtoto wa kocha huyo Michael Bradley anayecheza soka katika kilabu cha Borussia Moenchengladbach nchini Ujerumani.

FLASH-GALERIE Kombobild Kevin Prince Boateng und Jerome Boateng
Prince Boateng (kushoto) na Jerome BoatengPicha: picture alliance/dpa

Lakini kazi itakuwa kwa ndugu wawili wa baba mmoja lakini mama mbali mbali Jerome Boateng wa Ujerumani na Kevin Prince Boateng atakayekuwa akitetea nchi alikozaliwa baba yake Ghana. Wote ni wa baba mmoja lakini mama tofauti wa Kijerumani.

Kevin Prince atakayechezea Ghana mjomba wake ni Helmut Rahn, ambaye alifunga goli la ushindi kwa Ujerumani katika fainali ya kombe la dunia mwaka 1954. Mbali na historia ya mashindano haya kufanyika katika bara la Afrika, kuna historia nyingi zitakazoandikwa katika fainali hizi 2010 nchini Afrika Kusini.

Mwandishi: Böettcher, Arnulf / ZR / Sekione Kitojo.

Mhariri : Josephat Charo