Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika ya CHAN yaendelea
22 Januari 2018Mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani yanaendelea , ambapo wenyeji Morocco waliambulia sare ya bila kufungana na Sudan na kujiweka kileleni mwa kundi A la mashindano hayo.
Guinea , ambayo iliachana na kocha wake Kanfory Lappe Banguora baada ya kuondolewa kutoka katika kinyang'anyiro hicho Jumatano iliyopita, ilichukua nafasi ya tatu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania katika mchezo uliochezwa mjini Marrakech.
kocha wa Morocco Jamal Sellami alifanya mabadiliko ya wachezaji 10 katika kikosi chake kilichopambana na Guinea siku nne zilizopita, ambapo mshambuliaji mwenye mabao matano Ayoub el Kaabi akiwa miongoni mwa wale waliopumzishwa.
Morocco wenyeji wa mashindano hayo watapambana na timu ya pili katika kundi B, huenda Namibia , Jumamosi ijayo muda mfupi kabla ya Sudan kuoneshana kazi na mshindi wa kundi B , ambao huenda ni Zambia mjini Marrakech. Namibia na Zambia zimefanikiwa kufuzu kutoka kundi B baada ya ushindi mara mbili kila mmoja na zinakutana mjini Casablanca leo Jumatatu kuamua ni timu gani inashika nafasi ya kwanza.
Nae kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri Hector Cuper anatarajiwa kuiacha timu hiyo baad ya kombe la dunia mwaka huu. Meneja wa timu ya taifa ya Misri Eihab Laheita amesema kocha huyo raia wa Argentina amepokea maombi kadhaa ya kazi, lakini amekataa kuzitaja timu zinazomtaka.
Tangu alipochukua uongozi wa timu hiyo mwaka 2015 , Cuper aliiongoza Misri hadi kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990. Mwaka jana aliifikisha timu hiyo katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika AFCON baada ya mabingwa hao mara saba kushindwa kufuzu kucheza katika fainali hizo tangu mwaka 2010. Kabla ya kuchukua kazi ya kuifunza Misri , Cuper mwenye umri wa miaka 62 alifundisha klabu mbali mbali , hususan nchini Italia na Uhispania.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / rtre / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga