1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya ligi kuu ya soka Ujerumani Bundesliga kufikia ukingoni Jumamosi na bingwa wa soka Uingereza kujulikana Jumapili.

Mohamed Dahman9 Mei 2008

Wakati ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga inalenga nafasi kushiriki kombe la UEFA na kukwepa kushuka daraja bingwa wa soka nchini Uingereza aidha itakuwa Manchester United au Chelsea.

https://p.dw.com/p/Dx6h
Timu ya Manchester United pichani inawania kuwa bingwa wa soka nchini Uingereza kwa mara ya 17.Picha: AP

Mapambano ya kujiepeusha kushushwa daraja na kuwania nafasi ya michuano ya kombe la UEFA msimu ujao yanapamba moto hapo Jumamosi wakati ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga ikifikia ukingoni.Nchini Uingereza bingwa wa soka kujulikana Jumapili wakati Manchester United itakapokwaruzana na Wigan Athletic na Chelsea itakapokuwa mwenyeji wa Bolton Wanderes.

Timu ya Werder Bremen na Schalke hivi sasa zinawania nafasi ya mshindi wa pili katika michuano ya ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga nyuma ya Bayern Munich kuona ni timu gani kati ya hizo mbili itasonga moja kwa moja kwa kushiriki michuano ya klabu bingwa Ulaya.

Timu mbili za kwanza za Ujerumani zitaingia kwenye awamu ya makundi ya ligi ya klabu bingwa barani Ulaya msimu ujao wakati timu itakayoshika nafasi ya tatu itabidi ishiriki michuano ya kuwania nafasi ya kushiriki katika ligi hiyo.

Ushindi wa Bremen wa bao 1- 0 dhidi ya SV Hamburg wiki hii umeiweka kwenye nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 60 ikiwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya Bayern na pointi mbili mbele dhidi ya Schalke ambayo mapema wiki hii iliangusha Boschum kwa mabao 3-0.

Timu zote mbili zina mechi ngumu dhidi ya timu zenye umahiri wa soka wa kiwango cha wastani katika ligi wakati Bremen ambayo wachezaji wake wawili wametolewa nje katika mpambano wao na Hamburg itamenyana dhidi ya Hanover timu ya Schalke itacheza na Eintracht Frankfurt.

Nyuma yao kuna timu nne zinazowania nafasi ya kushiriki michuano ya kombe la UEFA zikiongozwa na Hamburg na Stuttgart zenye pointi 51 na Bayern Levekursen na Wolfsburg zenye pointi 48 kila moja.

Hamburg itapambana na Energie Cottbus ambapo ushindi utatosha kuwabakisha juu.

Leverkusen nayo itapambana na Hansa Rostock ambayo hata kama itashinda inabidi matokeo mengine yawe kwa faida yao kuepuka kushushwa daraja.

Katika mpambano wa kuepuka kushushwa daraja timu inayoshika nafasi moja kabla ya mwisho Duisburg inakumbana na mabingwa wapya wa ligi hiyo Bayern wakati Nuremberg itapambana na Hertha na Arminia Bielefeld itajimwaga dhidi ya Borussia Dortmund.

Karlsruhe inakutana na Bochum katika pambano jengine ambalo halihusishi masuala ya kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya UEFA wala kuepuka kushushwa daraja.

Mapambano ya kuwania ubingwa wa soka wa Uingereza yanasubiriwa kwa hamu.

Baada ya michezo 37 na miezi tisa ya kufanikiwa na kuharibikiwa michuano ya kuwania ubingwa wa ligi kuu ya soka nchini Uingereza inafika hatima yake hapo Jumapili kwa Manchester United kumenyana na Wigan Athletic wakati Chelsea ikikwaana na Bolton Wanderers kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa yenye hadhi na muruwa.

Wakati kukiwa kumebakia duru moja ya mwisho kabla ya kumalizika kwa michuano hiyo timu hizo mbili zinalingana pointi kila moja ikiwa ina pointi 84 lakini mabingwa watetezi Manchester United ina wingi wa magoli ambayo ni 17 zaidi dhidi ya Chelsea.

Manchester itakuwa mabingwa wa Uingereza kwa mara ya 17 na kulinyakuwa kombe la ligi kuu ya Uingereza kwa mara ya 10 iwapo watashinda mpambano wao huo. Liverpool ambayo mara ya mwisho ilishinda ubingwa huo hapo mwaka 1990 imevunja rekodi ya kuwa mabingwa wa Uingereza kwa mara 18.

Chelsea imewahi kushinda ubingwa huo mara moja tu hapo mwaka 1954- 1955 iwapo watakuwa mabingwa hapo Jumapili itakuwa ni mara ya tatu kutwaa kombe la ligi katika kipindi cha misimu minne.

Manchester imewahi kuwafunga Wigan mata tatu mabao 4-0 ukiwemo msimu huu wa ligi.

Na hatimae kidogo tuwadondolee mawili matatu juu ya tenis.

Mchezaji tenis nambari moja duniani Justine Henin alitolewa nje ya michuano ya Wazi ya Tenis nchini Ujerumani na Diana Safina katikati ya wiki hii kwa kushindwa kwa seti 5-7,6-3 na 6-1 katika duru ya tatu.

Matokeo hayo yamemaanisha kwamba kushindwa kwa bingwa huyo wa michuano ya wazi ya tenis ya Ufaransa na mchezaji wa Urusi kumemkosesha robo fainali iliokuwa ikisubiriwa kwa hamu dhidi ya bingwa wa zamani wa tenis duniani Serena Williams wa Marekani.